Idara ya Afya Mkoa wa Kigoma imejipanga kuendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na changamoto za vifo vya wanawake wajawazito, watoto wachanga pamoja na kufuatilia visababishi vya vifo hivyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba, amesema kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2022 hali ya vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi mkoani hapa ikiwa ni wanawake 85 pamoja na watoto wachanga 632.
Amezitaja baadhi ya sababu za vifo hivyo kuwa ni kifafa cha Mimba, Shinikizo la Damu, kuharibika kwa mimba, Marelia kali, wajawazito kutokamilisha matibabu, kutohudhuria kliniki kwa mfululizo pamoja na umbali kutoka kwenye Makazi hadi maeneo ya kutolea huduma za Afya.
‘‘Changamoto ya uhaba wa magari ya kusafirisha wagonjwa, baadhi ya maeneo kutofikika kwa urahisi nyakati za Masika, pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu tahadhari za kiafya kwa Mama wajawazito zimeendelea kusababisha ongezeko la vifo hivyo mkoani hapa’’ alisema.
Baadhi ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Idara ya Afya Mkoani Kigoma katika kukabiliana na vifo vya wanawake na watoto ni pamoja na kuongeza huduma za vituo vya upasuaji na uzazi, kutoa mafunzo kwa watoa huduma za uzazi, kuimarisha mfumo wa usafirishaji wagonjwa, kuimarisha huduma ya kliniki mkoba pamoja na kuongeza watumishi wa kujitolea na mikataba.
Amezitaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kufanya zoezi la kufuufuatiliaji wa kina na kuendelea kufanya utafiti ili kubaini sababu za vifo vinavyotokea katika Jamii na vituo vya kutolea huduma, hususani vinavyowahusu wanawake na watoto na kuchukua hatua stahiki.
‘’Tunaendelea kufanya zoezi la ukusanyaji wa Damu salama, kuanzisha vitengo vya huduma za Dharura kwa watoto wachanga na kuelimisha jamii kuhusu tahadhari mbalimbali kwa ajili ya usalama wa Mama wajawazito na watoto wachanga’’alisema Lebba.
Baadhi wa wakina mama wamekiri kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa Elimu ya Afya kwa jamii katika kutoa msaada kwa mama wajawazito hususani wanapokuwa katika hali ya ujauzito hadi wakati wa kujifungua.
‘‘Kumekuwa na Ushirikiano hafifu katika jamii hususani nyakati za kujifungua, jamii inatakiwa kubadilika ili kuongeza ushrikiano hali itakayonusuru changamoto mbalimbali zinazowakabili mama wajawazito na kusababisha vifo hivyo’’ Amesema Debora Mwampeta.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa