Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Mhe. Hassan Rugwa amesema Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa yenye mazingira rafiki kiuwekezaji nchini kutokana na hali yake kijiografia, kuendelea kuimarika kwa miundombinu ya uchukuzi na kutolea huduma za jamii pamoja na kupakana na nchi jirani za Burundi, Congo DR na Zambia.
Mhe. Rugwa ametoa kauli hiyo alipozungumza wakati akifungua semina ya uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani mkoa wa Kigoma iliyolenga kujadilina kubainisha fursa zilizopo mkoani hapa, iliyoratibiwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na kufanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Amesema serikali ya awamu ya Sita imewekeza zaidi ya Shilingi Tril.12 mkoani Kigoma kwa ajili ya kuchechemua uchumi wa Mkoa na wananchi kwa ujumla kupitia fursa zilizopo kupitia uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya kutolea huduma za jamii, uchukuzi na usafirishaji pamoja na kuimarisha masoko ya kimkakati.
Rugwa amesema amezitaja fursa hizo kuwa zipo katika sekta ya Kilimo, Uvuvi, biashara, mifugo sambamba na uwekezaji kupitia viwanda mbalimbali.
Amewaeleza washiriki wa semina hiyo kuwa, uhitaji wa nchi ya Congo DR katika kusafirisha mizigo hufikia Kontena 5000 huku hali halisi ya uwezo wa nchi ni kusafirisha chini ya Kontena 1400 kwa mwaka.
Aidha amesema kiwango halisi cha uhitaji wa abiria kusafiri baina ya Tanzania na Congo ni watu 8000 huku uwezo uliopo ni kusafirisha abiria 3000 kwa Mwaka.
‘’Nitumie nafasi hii kuwahimiza kuzitazama fursa hizo ili wafanyabiashara muweze kuwekeza katika maeneo hayo kutokana na serikali kuandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya kufanimisha uwekezaji wenu’’ amesema Rugwa.
Amesema barabara zinazouunganisha mkoa na mikoa jirani zimeshakamilika kwa kiasi kikubwa huku usafiri wa anga ukiendelea kuimarika kufuatia serikali kufanya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma kutoka Km 2 hadi kufikia Km.3.5 ili kuruhusu ndenge za kimataifa kutua mkoani Kigoma.
Upande wa Ardhi, Mhe Rugwa amesema sambamba na mkoa kuwa na maeneo mengi ya wazi yanayoruhusu kufanya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda au kuanzisha Kilimo cha mazao ya kimkakati, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetenga kiasi cha hekta 140 kwa ajili ya uwekezaji katika eneo maalum la uwekezaji la mkoa (Kigoma Special Economic Zone-KiSEZ)
‘’ Niwahimize wafanyabiashara kuwekeza katika kilimo cha zao la chikichi ili kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kupikia ndani na nje ya mkoa sambamba na kuwekeza kwenye ardhi kama walivyofanya wawekezaji katika kiwanda cha Sukari Kasulu’’amesema.
‘’Upande wa Afya, Serikali inajenga Hospitali ya Kanda sambamba na Tawi la Chuo Kikuu cha Muhimbili ambacho kitakuwa na wanafunzi kati ya 3000 hadi 10,000, idadi hiyo ya wanachuo ni kubwa sana hivyo itatoa fursa ya kiuchumi kwa wenye nyumba za kupangisha pamoja na wafanyabiashara ndogondogo’’ amesema Rugwa.
Amesema sambamba na hayo serikali iko kwenye hatua za mwisho kuunganisha mkoa na gridi ya Taifa ili kutatua changamoto ya muda mrefu ya kutotosheleza kwa umeme mkoani Kigoma.
Upande wake mshiriki wa Semina hiyo ambaye pia ni mfanyabiashara mkoani hapa Mousen Abdallah ameishauri serikali kupitia kikao hicho kukutana na wafanyabishara wa nchi jirani ya Congo DR ili waweze kujadili na kuondoa changamoto mbalimbali za kibishara.
Aidha ameiomba serikali kuandaa mafunzo ya pamoja baina ya wafanyabiashara wa Kigoma yatakayolenga kuwajengea uwezo katika kutambua majukumu ya Kituo cha uwekezaji cha Taifa jambo litakalowapa fursa ya kutambua namna bora ya kukopa na kuendesha mitaji yao kwa kuzingatia kanuni mbalimbali za kwa faida.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa