Maonesho ya Kitaifa ya Shirika la Viwanda Vidogo SIDO yanatarajiwa kufanyika Mkoani Kigoma mwezi septemab 2021 katika Halmashauri ya Kasulu.
Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amesema SIDO imeweka utaratibu wa kufanya maonesho ya kitaifa kila mwaka, ambapo tayari maonesho ya kwanza yalifanyika mkoani Simiyu, ya pili yalifanyika mkoani Singida na ya tatu yamepangwa kufanyika Wilayani Kasulu mkoani Kigoma kwa siku 10 kuanzia tarehe 21 hadi 30 Sptemba, 2021.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma itashirikiana bega kwa bega na SIDO kufanikisha maonesho hayo. Inatarajiwa wajasiriamali wapatao 700 wakiwemo kutoka nchi za jirani Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na kwingieko wanaotengeneza bidhaa mbalimbali za uhandisi, usindikaji vyakula, nguo, bidhaa mchanganyiko watahudhuria. Aidha Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za kiserikali zipatazo 40 zinazotoa huduma zitahudhuria maonesho hayo.
Muhimu ni kuwa SIDO Mikoa yote ya Tanzania bara watahudhuria wakileta teknolojia/ mashine mbalimbali zinazorahisisha uchakataji wa mazao na vitu mbalimbali.
“Nitoe wito kwa Halmashauri zote na Taasisi zote za Serikali na zisizo za Kiserikali, Miradi ya maendeleo, Makampuni makubwa na madogo yaliyopo mkoani Kigoma kushiriki ipasavyo katika maandalizi ya maonesho haya. Pia natoa hamasa kwa wajasiriamali na wananchi wote kushiriki katika maonesho kwa kuwa yatalenga kufungua fursa katika mkoa wa Kigoma” amesema Mkuu wa Mkoa.
Ametaja kuwa maonesho hayo yanalenga mambo mambo mbalimbali ikiwemo kutangaza shughuli na huduma za SIDO pamoja na wadau mbalimbali kwa wananchi ili wanufaike nazo, Kuhamasisha ubora wa bidhaa, kupanua soko na kutangaza bidhaa za wazalishaji wadogo wa ndani, kuona na kuonesha teknolojia mbalimbali ambazo ni zetu, rahisi, muafaka na rafiki wa mazingira
Ameongeza kuwa waoneshaji watapata fursa ya kuuza bidhaa zao na kujenga mahusiano na umoja wa kibiashara miongoni mwa wazalishaji, wafanyabiashara, wakulima na taasisi mbalimbali pia kuwawezesha wenyeviwanda vidogo kujifunza miongoni mwao na hatimaye kuzalisha bidhaa bora na zinazohimili ushindani na kukubalika katika soko.
Aidha katika maonesho hayo yatawawezesha wajasiriamali wazalishaji wadogo kubadilishana uzoefu na ujuzi wa kiufundi na kibiashara na kuwaunganisha wajasiriamali wadogo na wakubwa ili waweze kushikiana kibiashara na hatimaye kuwepo kwa sura nzuri ya uzalishaji mali nchini.
Amewaomba na kuwasisitiza wananchi kujipanga kupokea ugeni na kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazopatikana ili Mkoa wetu wa Kigoma uzidi kusonga mbele kimaendeleo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa