Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani hapa kuhakikisha wanakamilisha miradi yote ambayo serikali imekwisha kuielekezea fedha kwa ajili ya Utekelezaji wake.
Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Kigoma kilichofanyika Leo Februari 24, 2025 ambapo kupitia kikao hicho wajumbe wameazimia kumpongeza na kumuunga mkono Rais. Dkt. Samia Suluhu kwa kazi nzuri ya kuelekeza fedha nyingi mkoani hapa kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo.
Kupitia kikao hicho Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa watendaji katika Halmashauri za mkoa kuibua vyanzo vipya vya makusanyo ili kuziwezesha halmashauri kumudu kujiendesha sambamba na kutekeleza baadhi ya miradi ya Maendeleo.
Awali akizungumza na wajumbe wa kikao hicho, Naibu Waziri OR- TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba amesema takwimu zinaonesha Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza katika kupokea fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo ambapo mpaka sasa Jumla ya Tsh. Tril.11.5 zimekwisha pokelewa.
Aidha Waziri Katimba ameusisitiza uongozi wa Halmashauri kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato sambamba na kutengeneza mazingira wezeshi kiuchumi kwa wakazi mkoani hapa.
Akiwasilisha Taarifa ya Makadirio ya Mpango na Bajeti ya Mkoa kwa Mwaka 2025/2026 Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma Frank Chalres amesema kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 mkoa umekadiria kutumia kiasi cha Shilingi 308,288,177,736.
Amefafanua kuwa Shilingi 208,544,250,577 zitatumika kwa matumizi ya kawaida huku Shilingi 99,743,927,159 zitatumika kutekeleza miradi ya Maendeleo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Wabunge wa Mkoa wa Kigoma, Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama Mkoa, Makatibu Tawala wilaya, Wakurugenzi na wataalam kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wataalam kutoka Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na viongozi wa vyama vya Siasa mkoa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa