MKUU WA WILAYA YA KIGOMA SALUM KALLI AKIZUNGUMZA NA WAJUMBE (HAWAPO PICHANI) WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MKOANI KIGOMA. UZINDUZI HUO UMEFANYIKA LEO NOVEMBA 28, 2023 KATIKA UKUMBI WA OFISI YA MKUU WA MKOA WA KIGOMA.
AFISA MAENDELEO YA JAMII OFISI YA MKUU WA MKOA WA KIGOMA MSAFIRI NZUNURI AKIZUNGUMZA WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA KWA MKOA WA KIGOMA.
KAIMU KATIBU TAWALA MKOA WA KIGOMA ELISANTE MBWILO AKIZUNGUMZA NA WADAU WALIOJITOKEZA KUSHIRIKI UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA KWA MKOA WA KIGOMA ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA OFISI YA MKUU WA MKOA KIGOMA.
WADAU WA KAMPENI YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MKOANI KIGOMA WAKIFUATILIA HOTUBA YA MKUU WA WILAYA YA KIGOMA SALUM KALLI ALIPOKUWA AKIZUNGUMZA WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI HIYO YA SIKU 16 MKOANI KIGOMA.
Wakazi mkoani Kigoma wametakiwa kushiriki katika kupinga ukatilia dhidi ya wanawake na watoto kwa kutoa taarifa zItakazosaidia kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya makundi hayo ili kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.
Wito huo umetolewa Leo Novemba 28,2023 na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli alipozungumza akimwakilisha Mkuu wa Mkoa kuzindua Kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa Mkoa wa Kigoma.
Amesema waathirika wakuu wa madhara yatokanayo na vitendo vya ukatili wa kijinsia ni wanawake na watoto kutokana na jamii kutodhibiti tabia zisizozingatia usawa wa kijinsia na haki za binaadamu kwa makundi hayo.
‘’Tumeendelea kushuhudia vitendo vya utelekezaji wa familia, dhuluma katika mali za familia, ajira za watoto, unyanyasaji wa wanawake ndani ya ndoa pamoja na watoto wa kike kunyimwa haki zao za msingi katika familia na jamii kwa ujumla, mambo haya hayakubaliki na tunapaswa kuyapinga’’ amesema Kalli.
Mkuu huyo wa wilaya amewataka wanawake kutosita kujitokeza na kutoa taarifa kwa uongozi na vyombo vya usalama pale wanapokabiliwa na madhila yanayohusisha aina yoyote ya ukatili wa kijinsia.
‘’Baadhi ya wanawake wamekuwa wakibakwa hususani wakiwa katika maeneo ya mashambani lakini kutokana na kuogopa kuaibika au kutopewa kipaumbele kwa changamoto zao katika jamii, huamua kukaa kimya jambo linalohatarisha usalama wao wa Afya ya mwili na Akili’’ amesisitiza Kalli.
Kupitia Maadhimisho hayo yaliyoanza kitaifa Novemba 25 hadi Desemba 10, 2023, Mkuu wa Wilaya amewasisitiza wataalam kuhakikisha wanafika na kufikisha ujumbe wa maadhimisho katika maeneo yote ya mkoa wa Kigoma hususani vijijini ambapo vitendo hivyo vimekithiri.
Akiwasilisha taarifa ya shughuli zinakazofanyika katika siku 16 za maadhimisho, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma Msafiri Nzunuri amesema lengo mahususi la maadhimisho hayo ni kuungana na wadau ili kupata nguvu ya pamoja katika kuhimiza na kushawishi jamii kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kufikia usawa.
Nzunuri amezitaja shughuli zinazofanyika kipindi cha kampeni ikiwa ni ufikishaji elimu na hamasa kupitia vyombo vya habari, kufanya mikutano na wananchi pamoja na kusikiliza kisha kutatua changamoto zinazohusu ukatili wa kijinsia.
Aidha ameisisitiza jamii kuwekeza katika kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kwa kuwa ni kundi ambalo linapitia changamoto nyingi ikiwemo mgawanyo wa majukumu katika familia, mila na desturi kandamizi, ukosefu wa ujuzi na umasikini.
Pia amebainisha changamoto nyingine zinazokabili kundi hilo ni athari zitokanazo na changamoto za ubora na utoshelevu wa miundombinu nchini pamoja na ukubwa wa wategemezi katika kaya.
Kadhalika Nzunuri amesema matarajio ya Serikali pamoja na wadau ni kuhakikisha wanawake wanapata uelewa kuhusu masuala ya kijinsia, kupungua kwa idadi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na jamii kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.
Upande wake Katibu wa Kamati ya Maridhiano ya Dini mkoa wa Kigoma Padre Castus Rwegoshora amesema upande wao kama wahudumu wa masuala ya kiimani wanaendelea kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimiana na kuchukualina ili kudumisha hadhi na upendo kati ya wanadamu.
Pia ameishukuru serikali kwa kuendelea kutambua na kuchukua hatua dhidi ya changamoto ya uwepo wa vitendo vya ukatili miongoni mwa wanajamii.
Uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, umehudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Elisante Mbwilo, wakuu wa Sehemu na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, viongozi wa Madhehebu ya Dini pamoja na wadau kutoka Taasisi za Umma na Binafsi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa