MKUU WA WILAYA YA KIGOMA SALUM KALLI AKIZUNGUMZA NA WAKAZI WA MKOA WA KIGOMA SAMBAMBA NA MADAKTARI BINGWA NA WATENDAJI WENGINE WA IDARA YA AFYA WALIOHUDHURIA KWENYE UZINDUZI WA KAMBI YA MATIBABU YA MADAKTARI BINGWA WA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN MKOANI KIGOMA.
Na. Gladness Kusaga-Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli ametoa wito kwa wakazi ndani wa ndani na nje ya Mkoa wa Kigoma wenye changamoto za kiafya kuhudhuria Kambi maalum ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan inayolenga kutoa huduma za kibingwa za kimatibabu iliyozinduliwa katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni Kigoma leo Mei 6, 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kalli amesema Serikali kupitia madaktari hao bingwa wa magonjwa mbalimbali, imejipanga kuwafikia wagonjwa wote watakaohudhuria katika kambi hiyo na kuwapatia matibabu.
Amefafafanua kuwa, Hospitali ya Rufaa Maweni Kigoma kupitia Idara ya Afya Mkoa, imepokea madaktari bingwa sitini (60) kutoka Kanda mbalimbali ambao watakuwa tayari kutoa huduma kwa wagonjwa watakaojitokeza hadi katika muda wa ziada ili kuhakikisha wote wanaguswa na huduma hiyo.
Kalli ameishukuru Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Maweni kwa kuwaalika madaktari bingwa kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za kiafya kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma na maeneo jirani.
Naye Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Albert Paschal amesema mkoa umekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kupata huduma za kibingwa kwa ukaribu hivyo wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo ili kuepuka gharama ya kufuata huduma hizo katika mikoa mingine.
Ametoa wito kwa Wataalam wa Afya watakaoshiriki zoezi hilo kuzingatia miiko ya utoaji wa huduma ya Afya na Taaluma ya matibabu sambamba na kuviomba vyombo vya Habari kushiriki katika kusaidia kutoa taarifa kwa jamii ili wananchi wafahamu kuhusu uwepo wa kambi hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Maweni Kigoma, Dkt. Stanley Binagi amesema katika kipindi cha Siku tano za Kambi hiyo zitatolewa huduma bobezi za matibabu ya Pua, Koo, uchunguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi na matiti na changamoto za ugonjwa wa Moyo.
Amezitaja huduma nyingine kuwa ni upasuaji kwa ajili ya matibabu ya mifupa, matibabu ya kibingwa ya Moyo, uzazi kwa kina mama na kina baba, matibabu ya kibingwa ya moyo kwa watoto waliozaliwa na tatizo hilo, ngozi, figo pamoja na maradhi mengine ya ndani.
Aidha kupitia Kambi hiyo, Dkt. Binagi amesema wenye changamoto za macho na kuhitaji miwani watapatiwa bure, kufanyika kwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya akili sambamba na msongo wa mawazo.
Kambi hiyo ya Siku tano ya matibabu ya madaktari bingwa itakuwepo kuanzia leo Mei 6, 2024 ikihusisha madaktari kutoka Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Hospitali ya Kitete ya Tabora, Katavi na Sumbawanga.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa