Tabia ya Ulaji usiozingatia makundi Maalum ya Vyakula yenye virutubisho muhimu kwa Afya umetajwa kuchangia kuendeleza uwepo kwa hali ya utapiamlo, uzito pungufu, ukondefu na udumavu kwa watoto mkoani Kigoma.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Mhe. Albert Msovela alipozungumza kwenye Kikao Jumuishi cha Lishe Ngazi ya Mkoa kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2023 kilichofanyika mkoani hapa.
Amesema Mkoa unazalisha vyakula lishe vya kutosha lakini bado kumekuwepo na changamoto ya utapiamlo mkali pamoja na udumavu unaoathiri watoto na wanawake wajawazito, kutokana na jamii kushindwa kuzingatia ulaji unaohusisha makundi muhimu ya vyakula.
‘’Nitoe Wito kwa wataalam wa Afya, kuongeza nguvu katika kutoa Elimu ya Lishe kupitia majukwaa mbalimbali ili wananchi waweze kutambua umuhimu wa mlo kamili kwa lengo la kusaidia kukabiliana na hali ya utapiamlo na udumavu mkoani hapa’’ amesisitiza Msovela.
Msovela amewaelekeza Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya Mkoa kufanyia kazi Taarifa na takwimu za hali ya Afya na upatikanaji wa chakula zinazotolewa na watendaji ngazi za wilaya ili kubaini uweli wa Taarifa hizo na kuzifanyia kazi kuendana na uhakisia wake.
Ameitaka Timu hiyo kuendelea kukutana na wadau wanaotekeleza Afua mbalimbali za Afya mkoani Kigoma kwa kila robo Mwaka na kuweka wazi mikakati yao pamoja na hatua wanazochukua katika utekelezaji wa Afua hizo.
Pia Msovela ameielekeza Idara ya Elimu Msingi na Sekondari kuhakikisha utaratibu wa wanafunzi kupata Chakula shuleni unatekelezwa kwa asilimia mia moja pamoja na kuwataka kufuatilia na kufahamu hali ya ubora wa chakula kinacholiwa na wanafunzi katika shule za Sekondari za Bweni zilizopo mkoani hapa.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba amesema Idara ya Afya kupitia wataalam wa Lishe wameendelea kutoa Elimu ya utambuzi, uandaaji, utunzaji na ulaji wa makundi mbalimbali ya chakula ili kudumisha utamaduni wa kula mlo kamili.
Amesema iwapo walaji watatambua na kuzingatia muhimu wa kula vyakula kuendana na makundi yenye virutubisho Muhimu, Jamii itaachana na tabia ya kula vyakula kutokana na urahisi katika upatikanaji wake bali kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya kiafya mwilini.
Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Afua za Lishe, Afisa Lishe Mkoa James Ngalaba amesema hali ya udumavu kimkoa kwa Mwaka 2022 ilikuwa ni watoto 119,864 sawa na asilimia 27.1, udumavu uliokithiri watoto 38,480 sawa na Asilimia 8.7, uzito pungufu 53,961 sawa na Asilimia 12.2, pamoja na ukondefu ikiwa ni watoto 11,057.6 sawa na Asilimia 2.5.
Akitaja mikakati wa kukabiliana na kupunguza changamoto za lishe, Afisa Lishe Mkoa amesema wameendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya usimamizi shirikishi wa mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma za Afya, kujenga uelewa kuhusu masuala ya lishe kwa watendaji pamoja na wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii na katia vituo vya kutolea huduma za Afya vya Serikali.
Ameendelea kuitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali wa Afua za Lishe pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji elimu hiyo katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa