Jamii mkoani hapa imetakiwa kuzingatia kanuni za usafi wakati wote ili kuepuka uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.
Rai hiyo imetolewa na Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Johson Gamba alipokuwa akichangia mada kwenye Kikao cha Kamati Jumuishi ya Lishe Mkoa kwa Kipindi cha Julai-Septemba 2022, kilichofanyika katika Ukumbi wa Katibu Tawala Mkoani hapa.
Amesema jamii imejenga tabia ya kuzingatia masuala ya usafi na kuchukua tahadhari mbalimbali yanapotokea magonjwa ya mlipuko na kisha athari za maradhi hayo zinapopungua hujisahau na kuzirejea tabia za awali, jambo linaloruhusu kuendelea kujirudia kwa maradhi hayo.
‘‘Katika maeneo mengi ya Taasisi za Serikali na zile Binafsi pamoja na yale yenye mikusanyika mikubwa ya watu, tahadhari za uwepo wa vitakasa mikono zimeanza kupuuzwa, aidha maeneo mengi ya mijini changamoto ya udhibiti na uhifadhi wa taka imeendelea kushuhudiwa, hali inayohatarisha usalama wetu kwa ujumla’’ amesema Gamba.
Dkt. Jesca Lebba ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, amesema Mkoa unaendelea kukabiliana na changamoto za kiafya ikiwemo suala la udumavu kwa kuendelea kutekeleza Afua mbalimbali za Lishe ikiwa ni pamoja na kuwaagiza wazabuni wanaolisha katika shule mbalimbali mkoani hapa kusaga mahindi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi hao katika mashine zenye utaratibu wa kuongeza virutubishi.
Ameeleza kuwa, wameendelea kuhamasihsa kilimo cha viazi lishe katika shule za Msingi za Sekondari zenye maeneo yanayoruhusu kilimo cha zao hilo ili kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula hicho na kujenga tabia ya kilimo cha zao hilo lenye manufaa makubwa kiafya.
Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai-Septemba 2022, Bi. Naomi Rumenyela amesema kuwa, utekelezaji wa Afua za lishe umefanyika kwa ufanyaji kazi za maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe, ukaguzi usalama wa chakula, upimaji wa chumvi, unasishi kwa wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii, kufuatilia zoezi la utoaji wa Fedha za kuratibu upatikanaji Lishe Shuleni na utioaji wa madini ya Foliki kwa wajawazito.
Aidha amesema shughuli za utoaji wa matone nyongeza ya Vitamini A, ulishaji wa watoto katika vituo vya kutolea huduma na kufanya maadhimisho ya ulishaji wa chakula shuleni yalifanyika kwa ukamilifu katika kipindi kilichopangwa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa