Wakazi mkoani Kigoma wameaswa kuzingatia ulaji unaojumuisha makundi mbalimbali ya vyakula ili kukabiliana na janga la utapiamlo na kujenga msingi wa Afya bora kwa watoto.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Nesphoty Sungu alipofungua kikao cha Kamati ya Lishe mkoa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2023, na kusisitiza kuwa pamoja na mkoa kuzalisha chakula cha kutosha bado kunachangamoto ya uwepo wa utapiamlo.
Amesema maeneo mengi ya mkoa yanazalisha aina mbalimbali za vyakula lakini changamoto kubwa inatokana na wakazi kujenga mazoea ya kutokula vyakula kwa kuzingatia mlo kamili hivyo kusababisha kuendelea kuwepo uwepo wa changamoto utapiamlo na udumavu.
Amesema Idara ya Afya Mkoa kupitia Kitengo cha Lishe imefanikiwa kupambana na kupunguza udumavu kutoka watoto 300,000 hadi 119,000 ikiwa ni sawa na kutoka Asilimia 43. Hadi kufikia 27.
Ameendelea kufafanua kuwa sambamba na suala la lishe Jamii inapaswa kusimamia suala la makuzi ya watoto ikiwemo kuwapa ulinzi dhidi ya vitisho na unyanyasaji ili kuwafanya waweze kuishi salama pamoja na kuwajengea ujasiri wa kuweza kukabiiana na changamoto mbalimbali katika mazingira yao.
Aidha Sungu ameisisitiza jamii kuendelea kukabiliana na janga la utapiamlo kwani husababisha madhara makubwa kwa watoto chini ya miaka mitano ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu pamoja na athari mbalimbali zitokanazo na maradhi yasiyotibika na kuiletea jamii mzigo mkubwa.
Akiwasilisha Taarifa ya utendaji kazi kwa Kipindi cha Julai hadi Septemba 2023, Mratibu wa Lishe Mkoa wa Kigoma James Ngaraba amesema katika kuhamasisha suala la lishe, mkoa unaratibu na kusimamia utaratibu wa kila kijiji kuadhimisha Siku ya lishe kila baada ya miezi mitatu.
Amesema kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2023 kiwango cha Shule zinazotoa chakula shuleni kimkoa kimefikia Asilimia 65.7, viwanda vinavyoongeza virutubishi kwenye chakula ikipanda kutoka Asilimia 37.5 hadi 51.1, huku ulaji wa chakula shuleni ukipanda kutoka Asilimia 65.7 hadi 68.2.
Ameendelea kufafanua kuwa katika kipindi hicho, idadi ya watoto waliogundulika na ukondefu imeshuka kutoka Asilimia 0.5 hadi kufikia 0.3, kilibatumbo kutoka Asilimia 0.3 hadi 0.1 na utapiamlo mkali kutoka Asilimia 0.5 hadi 0.4.
Afisa Afya Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni Francisca Lutumula amesema changamoto inayoikabili jamii ni kushindwa kuelewa dalili na Athari za utapiamlo hali inayosababisha madhara makubwa kwa watoto.
‘’Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kufahamu dalili na madhara yatokano ya upungufu wa lishe kwani baadhi wananchi huhusisha madhara hayo na Imani za kishirikina jambo linaloweza kuwaathiri watoto kwa kiasi kikubwa’’ amesema Francisca.
Wakichangia agenda mbalimbali zilizowasilishwa kupitia kikao hicho, wajumbe wameshauri Kitengo cha Lishe Mkoa kufuatilia, kubaini na kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa chumvi isiyo na madini joto.
Wamesisitiza watendaji wa kitengo hicho kuendelea kufuatilia na kuwabaini wazalishaji kisha kuwapa miongozo itakayowataka kuzingatia kuingiza sokoni chumvi itakayowekewa madini hayo muhimu kwa usalama wa Afya za walaji.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa