BAADHI YA MADIWANI, VIONGOZI WA SERIKALI NA WATUMISHI WA MANISPAA YA KIGOMA-UJIJI WAKIWA WAMEJIANDAA KUUPOKEA MWENGE WA UHURU KATIKA UWANJA WA SHULE YA SEKONDARI BURONGE, LEO TAREHE 30/SEPTEMBA 2022.
Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuzingatia Afua za Lishe katika kukabiliana na tatizo la udumavu kwa wakina mama na watoto ili Taifa liweze kuendelea kuwa na kizazi chenye afya bora.
Akikagua Huduma za Lishe kabla ya kuweka jiwe la Msingi katika Kituo cha Afya Buronge kilichopo Halmashauri ya Manispaa Kigoma-Ujiji Mkoani hapa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2022 Sahili Geraruma aliwataka wakazi kuyapa kipaumbele masuala ya Lishe ili kuimarisha Afya ya Mama, mtoto na Jamii kwa ujumla.
‘‘Suala la umuhimu wa Afya tunapaswa kulipa kipaumbele kwani bila kuwa na Afya bora hatutoweza kufanya kazi na kuuimarisha uchumi wetu binafsi na Taifa kwa ujumla’’alisema Geraruma.
Sambamba na ukaguzi huo, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge kitaifa, alipata fursa ya kukutana, kuzungumza kisha kutoa chakula chenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni Nne Fedha kutoka Halamshauri, kwa Konga la Halmashauri ya Manispaa Kigoma-Ujiji.
‘‘Kuishi na Virusi vya Ukimwi sio tatizo bali tatizo ni kutokuwa mfuasi sahihi wa dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo’’alisisitiza Geraruma.
Naye Mtaalam wa Masuala ya Lishe Dafroza Bernard, alisema makuzi ya akili na mwili wa mtoto hutegemea zaidi mlo kamili na wenye ubora.
‘‘Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo la udumavu na kwa kiasi kikubwa linachangiwa na baadhi ya wakazi kutokubali kuipokea elimu ya Afua za lishe na kuamua kubadilika ili kuzingatia Afua hizo’’
‘‘Nakiri kuwepo kwa changamoto za kiuchumi lakini hata wanaomudu kupata vyakula vya kutosha hawazingatii utaratibu wa kula mlo kamili’’ alisema Dafroza.
Upande wake Mwenyekiti wa Konga la Halmahsauri Manispaa Kigoma-Ujiji, Athumani Rajabu alisema wameguswa na tukio hilo la kutolewa kwa chakula huku akisisitiza jamii iendelee kufanya matendo yanayogusa utu kuliko unyanyapaa kwa wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Alisema tabia ya unyanyapaa imeendelea kujitokeza kwa baadhi ya watu wasio na Elimu kuhusu ugonjwa wa UKIMWI huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kutoa elimu pamoja na Dawa za kufubaza maradhi hayo.
‘‘Kwa sasa hatuna usumbufu wa kufuatilia dawa mara kwa mara kwani ukiwa mfuasi mzuri unaweza kupewa dawa za kutumia kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita kutegemeana na hali ya utoshelevu wa viini kinga mwailini’’ alisema Rajabu.
Mbio hizo za Mwnge wa Uhuru kwa Mwaka 2022 katika Halmashauri ya Manizpaa ya Kigoma-Ujiji, zimezindua, kutembelea, kuweka jiwe la msingi na kutoa chakula ambapo huduma na miradi hiyo ikiwa na Thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.6
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa