Jamii mkoani hapa imetakiwa kutumia fursa ya uwepo wa masanduku ya maoni yanayopatikana kwenye vituo vya Serikali vinavyotoa huduma za kijamii kwa lengo la kupaza sauti na kubainisha changamoto mbalimbali zilizopo katika maeneo wanayoishi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Rai hiyo imetolewa na Mshauri wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo katika Sekta za Umma Kanda ya Magharibi, Samwel Mashindika wakati wa kikao kazi kilicholenga kuwajengea uwezo baadhi ya wakuu wa Idara na vitengo vinavyohusika na utekelezaji wa Mradi huo katika kufuatilia Taarifa za utendaji kazi kilichofanyika Halmashauri ya wilaya ya Uvinza.
Amesema masanduku hayo yanatoa Uhuru kwa wananchi kufikisha Taarifa za kero na changamoto za utoaji na upatikanaji huduma katika taasisi za kiserikali na hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na kuleta matokeo chanya baada ya kupatikana kwa utatuzi wa changamoto hizo.
‘’Baadhi ya wananchi wamekua waoga kufika ofisini na kuwaambia wahusika moja kwa moja kuhusu changamoto zinazojitokeza katika utendaji kazi wao kwa kuhofia kuibuka kwa uhasama baina yao na wanaolalamikiwa, bali kupitia mfumo wa masanduku ya maoni, ujumbe huwafikia walengwa na maamuzi kufanyika bila kuathiri mahusiano ya pande zote mbili’’ amesema.
Mratibu wa Mradi huo wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3 Plus) Kanda ya Magharibi Bi. Rose Mwangilima, amesema Masanduku hayo yameendelea kuleta matokeo chanya kwa kung’amua kero mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwemo kutopatikana kwa huduma kwa ukamilifu, ukiukwaji wa haki za binaadamu na mapungufu katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kisheria.
Amesema Malalamiko mengi yanayotolewa na kushughulikiwa yamekuwa yakijitokeza katika Nyanja za Elimu, Afya, Utawala, Sheria pamoja na Usalama wa Raia.
‘‘Maoni hutolewa na wananchi kuendana na mahitaji yanayowagusa kama jamii na iwapo wahusika watayafanyia kazi na walengwa kukubali kuwajibika ama kuwajibishwa, kero nyingi za wananchi zitabainika, kufanyiwa kazi na kuondoa sintofahamu zinazojitokeza katika jamii’’ amesema Bi. Mwangilima.
Upande wake Afisa TEHAMA Mkoa wa Kigoma Bi. Ashura Sadick, ameshauri Taasisi zote za Serikali zihakikishe zinakuwa na Sanduku la Maoni pamoja Kamati hai zitakazohakikisha malalamiko yanapokelewa na kushughulikiwa kwa wakati. Aidha amesisitiza kuwa, watakaohusika na usimamizi wa masanduku hayo wawe huru kutekeleza wajibu wao bila kuingiliwa katika utendaji kazi.
PICHA: Wataalam wa Idara na vitengo mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Halmashauri ya wilaya Uvinza pamoja na waratibu wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3 Plus) Kanda ya Magharibi wakiwa katika Majadiliano wakati wa Kikao kazi kilichofanyika katika halmashauri ya Uvinza, kikiwa na Lengo la kuwajengea uwezo baadhi ya wakuu wa Idara na vitengo vinavyohusika na utekelezaji wa Mradi huo katika kufuatilia Taarifa za utendaji kazi kwa ngazi mbalimbali Serikalini.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa