Jamii wilayani kibondo mkoani Kigoma, imetakiwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti Marelia nchini kwa kutokwamisha zoezi linaloendelea la unyunyiziaji dawa ya kiuatilifu ukoko majumbani ili kudhibiti ugonjwa huo hatari.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alipozungumza na wakazi wa wilaya ya Kibondo, akiwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kutembelea na kukagua maendeleo ya zoezi la unyunyiziaji wa dawa hiyo katika wilaya za Kasulu na Kibondo ambazo Serikali inatekeleza zoezi hilo kimkoa.
‘‘Haiwezekani baadhi ya watu wasiruhusu miji yao kufikiwa na wanaofanya zoezi la kunyunyiza dawa, hii itatusababishia kuendelea kuwepo kwa mazalia ya mbu katika baadhi ya maeneo kisha wataanza kutusumbua mara baada ya kukamilika kwa zoezi hili’’amesema.
‘‘Marelia imeendelea kuwa ugonjwa unaosababaisha asilimia kubwa ya vifo vya watanzania huku idadi kubwa ikiwa ni kina mama na watoto. Hivyo kuunga mkono juhudi hizi za Serikali kutatusaidia katika kujihakikishia usalama wa maisha yetu na vizazi vyetu’’ amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Amesema maradhi huchangia kushusha ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kupunguza uwezo wa uzalishaji mali katika jamii zetu.
‘‘Unapouguza au kuugua huwezi kuendelea kufanya shughuli zozote za uzalishaji mali na usipopata matibabu sahihi na kwa wakati unaweza kupata ulemavu wa kudumu au kifo’’ amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Andengenye, amesisitiza wananchi kuendelea kupokea na kuzingatia maelekezo ya wataalam pamoja na kuachana na aina yoyote ya uvumi kuhusu uwepo wa madhara yatokananyo na matumizi ya dawa hiyo.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kibondo, wamekiri kushuka kwa kasi ya ugonjwa huo mara baada ya Serikali kuanza kutekeleza zoezi la Upuliziaji wa kiwatilifu ukoko majumbani katika makazi yao.
‘‘Kwa sasa hali ni tofauti na awali ambapo tulikuwa tukiugua marelia mara kwa mara, lakini tangu lianze zoezi hili la upuliziaji dawa, baadhi yetu imepita miaka mitatu bila kuugua ugonjwa huo’’ amesema Magreth mkazi wa Kitongoji cha Bitulana Mtoni, Kata ya Bitulana.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa