Jamii mkoani hapa imetakiwa kuchukua hatua za Makusudi katika kuhakikisha Mazingira yanakuwa salama kwa kuepuka kutupa taka ovyo na kuteketeza kwa usahihi zile zilizopo ili kudumisha Sera na mikakati endelevu ya kukabiliana na uharibifu wa Mazingira.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mazingira Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bi. Mercy Mbungulu alipoongoza zoezi la Usafi wa Mazingira katika Eneo la Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Kigoma kisha kutoa Elimu ya utunzaji wa Mazingira udhibiti wa taka ngumu, kwa baadhi ya wadau wa Mazingira ikiwa ni katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Mazingira Duniani.
Amesema katika wiki ya Maadhimisho hayo, wamejikita katika kutoa Elimu na kushiriki kufanya usafi wa Mazingira kwenye Maeneo yanayotoa huduma muhimu za kijaii yanayohusisha muingiliano mkubwa wa watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Mkoa.
‘’Leo tumeshiriki kufanya Usafi katika Eneo la Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Kigoma kwa sababu eneo hili ni kati ya Maeneo yanayoingiza wageni wengi mkoani Kigoma wakitokea ndani na nje ya nchi, hivyo tumefanya hivi ili kutoa hamasa na Elimu kwa watumishi wa eneo hili pamoja na wakazi wa Maeneo ya jirani na uwanja huu’’ amesema Mbungulu.
Amesisitiza kuwa ’’Tumetoa Elimu kuhusu udhibiti wa Mifuko ya Plastiki kwa vijana wa vyuo, katika maeneo ya Stendi, vituo vya Afya, Masoko pamoja na maeneo mengine ya kutolea huduma za kijamii ili kuongeza uelewa kuhusu madhara na umuhimu wa udhibiti wa bidhaa hizo zinazochangia uzalishaji wa taka ngumu’’
Mbunguru amefafanua kuwa, kilele cha Maadhimisho hayo ni muendelezo wa juhudi za Serikali mkoani Kigoma katika kufikisha Elimu na kuhamasisha suala la utunzaji wa Mazingira katika Jamii.
Naye Meneja wa Baraza la Taifa la uhifadhi wa Mazingira Kanda ya Magharibi Mkoa wa Kigoma Edgar Mgira, amesema moja wapo ya Jukumu wanalotekeleza kupitia Siku hiyo ni kutoa Elimu ya Usafi wa Mazingira kwa watumishi wa Uwanja wa ndege mkoa wa Kigoma pamoja na wadau wengine wa Mazingira kwa lengo la kupunguza Madhara yatokanayo na utupaji wa Taka ngumu ikiwemo mifuko ya Plastiki.
Ameongeza kuwa mpango mkakati uliopo ili kuimarisha na kujenga uelewa kwa wakazi mkoani hapa kuhusiana na usafi wa Mazingira ni pamoja na kutembelea wadau mbalimbali wa Mazingira katika maeneo yao pamoja na kutumia vyombo vya Habari kutoa Elimu na miongozo ya kudhibiti uchafuzi wa Mazingira.
Baadhi ya wadau wa Mazingira mkoani hapa walioshiriki zoezi hilo, wameiomba Serikali kupitia Mamlaka zinazosimamia uhifadhi na usimamizi endelevu wa Mazingira mkoani hapa, kulifanya suala la usafi kuwa endelevu badala ya kusubiri nyakati za Maadhimisho.
wamesema Suala la kuhamasisha usafi, kusimamia na hata kuwawajibisha wasiofuata taratibu zilizowekwa na Serikali linatakiwa kufanyika nyakati zote ili kudhibiti tabia Hatarishi kwa usalama wa Mazingira kwa ajili ya Maisha ya kizazi cha sasa na kijacho.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa