Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Lameck Mlacha ameiasa Jamii kujenga tabia ya kutatua migogoro yao na kuimaliza kwa njia ya usuluhishi nje ya mifumo ya Mahakama ili kuepuka upotevu wa fedha pamoja na muda ili kutumia rasilimali hizo katika kujiletea maendeleo.
Jaji Mlacha ametoa Rai hiyo alipozungumza kwenye hafla fupi ya Maadhimisho ya Kilele cha wiki na Siku ya Sheria ambayo kimkoa yamefanyika kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ngazi ya Mkoa na wilaya, Vyama vya Siasa, Dini, watumishi wa Idara ya Mahakama pamoja na wadau mbalimbali wa Sheria mkoani Kigoma.
‘‘Jamii iwe tayari kumaliza migogoro nje ya vyombo vya Sheria kwa sababu Fedha na Muda vinapotea kwa sababu ya kufuatilia kesi badala ya kufanya shughuli za maendeleo na matokeo yake baada ya upande mmoja kushindwa unaanza kujenga chuki na visasi hali inayoweza kuhatarisha amani na usalama. ’’amesema Jaji Mlacha.
Jaji huyo amezitaka Taasisi za Dini, vyombo vya Habari, Jeshi la Polisi pamoja na watendaji wa Mahakama kushirikiana katika kutoa Elimu na kuhamasisha umuhimu wa kutumia usuluhishi kama njia kuu ya kutatua na Kumaliza Migogoro pia Jamii imetakiwa kuwa tayari kujenga utamaduni wa kutafuta suluhu bila kufika kwenye vyombo vya Sheria.
‘‘Mtumie fursa ya nafasi mlizonazo katika kuhudumia Jamii kukutana na kuongea na wananchi juu ya umuhimu wa kutumia mbinu ya usuluhishi katika kutatua migogoro, kwani kwa kufanya hivyo mtajenga jamii yenye upendo, msamaha, ushirikiano na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla’’ amesisitiza Jaji.
Aidha Jaji Mlacha amefafanua kuwa Mwaka 2022 Mahakama zote mkoani Kigoma zilipokea na Mashauri 5366 ambapo yaliyoamuliwa kwa suluhu ni 256 sawa na Asilimia 4.8 na yaliyobaki yaliamuliwa na Mahakama kutokana na wahusika kukosa utayari wa kumaliza migogoro yao nje ya Mahakama.
Ameongeza kuwa, mkoa unachangamoto ya kukosa taasisi za nje ya Mfumo wa Mahakama zenye uwezo wa kuendesha vikao vya usuluhishi, baadhi ya Mahakimu kukosa utayari wa kujitolea kufanya usuluhishi, ukosefu wa Elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kumaliza migogoro bila kutegemea maamuzi ya kimahakama pamoja na tabia binafsi za baadhi ya wanajamii kutokubali kutoa msamaha kwa wanaowakosea.
‘‘Mahakimu mnawajibu wa kuwaelimisha wateja wenu kabla hawajaanza kusikiliza kesi zao kuhusu umuhimu wa kukaa na kusikilizana kisha kumaliza tofauti zao nje ya mahakama hususani kwa kesi zisizo za jinai, kwani hukumu za kimahakama zina machungu yake kwa upande wa anayehukumiwa’’ amesisitiza Mhe Jaji Mlacha.
Maadhimisho ya wiki na Siku ya Sheria Mwaka 2023 yameongozwa na Kauli mbiu isemayo ‘’UMUHIMU WA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI KATIKA KUKUZA UCHUMI ENDELEVU: WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU.
PICHA MBALIMBALI ZA HAFLA YA MAADHIMISHO YA WIKI NA SIKU YA SHERIA MKONI KIGOMA.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa