Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Asina Omari ametoa wito kwa wakazi mkoani hapa kujitokeza ili kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la kudumu la wapiga Kura Awamu ya pili zoezi ambalo limeanza tarehe Mosi Mei, 2025 kimkoa huku likitarajiwa kukamilika Mei 7, 2025.
Mhe. Jaji Asina Omari anesema hayo alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma akiwa katika ziara ya kukagua Maendeleo ya Utekelezaji wa zoezi hilo ngazi ya wilaya ambapo ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa kusimamia vizuri zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura awamu ya kwanza huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi badala ya kusubiri mpaka siku ya mwisho.
Amesema mkoa wa Kigoma una jumla ya vituo 277 kwa ajili utekelezaji wa zoezi hilo linaloenda sanbamba na uwekaji wazi daftari la awali la wapiga kura, vilivyopo katika ngazi za kata ambapo matarajio ya tume ni kuandikisha wapigakura wapya 74,122 huku wengine 24,323 wakitarajiwa kuboresha taarifa zao.
Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye amesema mkoa unaendelea kushirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
Sambamba na hayo amewakumbusha wakazi wa Kigoma kuona umuhimu kujitokeza na kushiriki zoezi hilo ili waweze kupata fursa ya kuchagua viongozi watakaowataka ambao pia watatokana na maamuzi yao halali kupitia upigaji kura.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa