Idara ya Elimu Sekondari kwa kushirikiana na wazazi Mkoani hapa wametakiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu Elimu ya Msingi wanajiunga na kuendelea na Masomo kwa ngazi ya Sekondari katika Muhula Mpya wa Mwaka wa Masomo wa 2023.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alipoanza Ziara yake ya kikazi wilayani Buhigwe ikiwa na lengo la kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa vyumba vya Madarasa ya Wanafunzi wanaotarajiwa kuanza Kidato cha Kwanza katika wilaya nane za Mkoa wa Kigoma.
Amesema wazazi kwa kushirikiana na wataalam wa Idara ya Elimu Sekondari wahakikishe wanaweka mikakati madhubuti yenye lengo la kufanikisha wanafunzi wote waliofaulu Elimu ya Msingi na kuchaguliwa kujiunga na Elimu ya Sekondari, wanafika na kuanza masomo katika Shule walizopangiwa ili waweze kupata haki hiyo ya kitaaluma.
‘‘Elimu ni haki ya Msingi kwa watoto wetu na ndio msingi wa ujenzi wa Taifa, hivyo hatua madhubuti zinatakiwa kuchukuliwa ili kujenga Taifa la watu wenye weledi kupitia upatikanaji na usimamizi mzuri wa kitaaluma kwa watoto wetu’’ amesema.
Aidha amewaagiza wasimamizi na mafundi wanaotekeleza jukumu la ujenzi wa madarasa hayo, kuongeza kasi sambamba na kusimamia ubora wa kazi.
Naye Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma David Mwamalasi, amesema Mkoa wa ulipokea Jumla ya Shilingi 7, 160, 000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 328 vya Madarasa ya Kidato cha kwanza kwa Mwaka 2023 ambapo utekelezaji wa shughuli za ujenzi ulianza Oktoba 2022 kwa Halmashauri zote nane za Mkoa.
Ameendelea kufafanua kuwa, mpaka sasa ujenzi uko katika hatua mbalimbali ambapo vyumba sita vipo katika hatua ya ukuta, 21 hatua ya Lenta, 175 hatua ya upauaji, 156 hatua ya umaliziaji na hakuna shughuli inayoonyesha mkwamo kwa kuwa katika maeneo yote mafundi wapo kazini na wanaendelea vizuri na kazi.
Akiwa wilayani Buhigwe, Mkuu wa Mkoa amekagua maendeleo ya ujenzi wa Madarasa hayo kwa ajili ya Wanafunzi wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza katika Shule za Sekondari Mnanila, Nyakimwe, Kibwigwa, Buyenzi, Muyama, Kahunga, Buha na Yanza.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa