PICHA MBALIMBALI ZA ZIARA YA UKAGUZI WA UTEKELEZAJI MRADI WA HUDUMA YA MSINDIKIZAJI MKOANI KIGOMA ILIYOFANYIKA JANUARI 18, 2023 KATIKA KITUO CHA AFYA KIGANAMO PAMOJA NA HOSPITALI YA WILAYA YA KASULU. MFADHILI NA MKURUGENZI MKUU WA MRADI WA HUDUMA YA MSINDIKIZAJI BI. HELLEN NA UJUMBE WAKE AKIAMBATANA NA MGANGA MKUU WA MKOA WA KIGOMA DKT. JESCA LEBBA NA NA WATAALAM WA AFYA WANAOSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MRADI HUO KIMKOA, WALIPATA FURSA KUTEMBELEA VITUO HIVYO, KUJIONEA UTEKELEZAJI, KUPOKEA CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA NA KUTOA USHAURI WA KUTATUA CHANGAMOTO HIZO.
Serikali mkoani Kigoma imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa Maendeleo katika Sekta hiyo ili kukabiliana na kutokomeza changamoto zinazowakabili Mama wajawazito na kuwahakikishia Mazingira Salama ili kulinda uhai wa Mama na Mtoto wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba alipofanya ziara katika Kituo cha Afya Kiganamo kilichopo wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, kwa lengo la kukagua Maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Huduma ya Msindikizaji unaotekelezwa chini ya Mradi Mama wa Thamini Uhai akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mradi huo Bi. Hellen Ageru na ujumbe wake.
Lebba amesema mafanikio yanayoendelea kujitokeza katika utekelezaji wa Mradi wa Huduma ya Msindikizaji ni ukombozi kwa Mama wajawazito kwani yamerahisha mawasiliano baina ya wajawazito na wahudumu inapotokea mjamzito ameshindwa kuomba msaada wa haraka kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa kujifungua ambazo zinaweza kuhatarisha uhai wa Mama mjamzito na Mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.
‘‘Jamii inapaswa kutambua kuwa Mama Mjamzito anapaswa kuangaliwa kwa ukaribu, kupatiwa faraja, pamoja na msaada wa tahadhari mbalimbali za kiafya ili aweze kujifungua kwa usalama na kulifanya zoezi la uzazi kutokuwa jambo hatarishi kwa uhai wa Mama na mtoto’’ Amesema Lebba.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa Huduma ya Msindikizaji unaotekelezwa chini ya Mradi Mama wa Thamini Uhai Bi. Hellen Ageru amesema ameridhishwa na Hali ya Utekelezaji wa Mradi huo katika Mkoa wa Kigoma na kusisitiza kuendelea kutolewa wito kwa Jamii ili muitikio uwe mkubwa.
Amesema suala la uendelezaji wa Mradi ni jukumu la Serikali kupitia wasimamizi na Jamii kwa ujumla kwa kuwa yeye hawezi kuwepo muda wote ambao Jamii itahitaji Huduma hiyo, hivyo ni wajibu wa wasimamizi hao kuandaa mazingira Mazuri ili kuhakikisha Mradi unaboreshwa na kuimarishwa.
‘‘Naamini Serikali, wadau pamoja na wananchi wanaotekeleza na kunufaika na huduma hiyo, watashirikiana kwa ukaribu kutatua changamoto mbalimbali zinazoonekana kujitokeza ili kuhakikisha mradi unaendelea kutekelezwa kuendana na malengo tuliyojiwekea’’ amesema Hellen.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi kwa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kiganamo Primus Ijuma, amesema kupitia Mradi huo, kituo kimefanikiwa kujenga miundombinu ya kujifungulia yenye uwezo wa kuhudumia kwa wakati mmoja Mama wajawazito sita wakiwa na wasindikizaji wao bila kuathiri utoaji huduma nyingine za kitaalam.
Ameeleza kuwa mradi umeendelea kuimarisha ushirikiano na kufanikiwa kupunguza uwepo wa malalamiko kwa jamii juu ya utendaji kazi kwa watoa huduma wa Afya kutokana na ushiriki msindikizaji ambaye huwajibika katika shughuli zote zisizo za kitaalam kama vile kumsaidia mama mjamzito kufanya mazoezi, kumpa ushauri wa kisaikolojia na matumaini ya kujifungua salama.
‘‘Kwa Mwaka 2022 utekelezaji wa Mradi wa umesaidia kupunguza vifo vya Mama wajawazito na watoto ambapo jumla ya waliofanikiwa kujifungua katika Kituo cha Afya Kiganamo ni wakina mama 1200 ambapo aliyefariki kwa sababau za uzazi ni mmoja na watoto wachanga waliofariki wakiwa tisa.
Mratibu Mkuu wa Mradi wa Thamini Uhai Nchini Banzi Msumi amemshukuru mfadhili wa Mradi huo na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kuigusa Jamii hususani katika kunusuru vifo vya Mama wajawazito na watoto pamoja na kujenga utamaduni wa kutoa msaada kwa kina mama hao.
Aidha amefafanua kuwa, Mradi huo unatekelezwa Mkoani Kigoma katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Kigoma pamoja na Mkoa wa Katavi, ambapo maeneo hayo yamethibitika kuwa na changamoto ya Jamii kutokuwa karibu na kutoa misaada mbalimbali isiyo ya kitaalam kwa Mama wajawazito hususani nyakati za kujifungua zinapokaribia.
‘‘Mradi huu upo katika Awamu ya Tatu ya Utekelezaji, ambapo awamu ya Kwanza ilianza 2016 na mpaka sasa tukiwa katika awamu hii ya Tatu Jumla ya vituo 15 vinatekeleza mradi mkoani Kigoma na nane kwa Mkoa wa Katavi.
Ameongeza kwa kusema, Jamii imeelishwa na kuongeza muitikio katika kuwasaidia mama wajawazito kabla na wakati wa kujifungua, ambapo kwa sasa wasaidizi wanapatikana katika maeneo ya vituo vinavyotekeleza Mradi pamoja na wale wanaotoka majumbani ambao huwa ni ndugu au jamaa wa Mama wajawazito.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa