Halmashauri Nane za Mkoa wa Kigoma zimefanikiwa kupata Hati safi za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mujibu wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Halmashauri hizo ni Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Mji Kasulu pamoja na Halmashauri za Wilaya Kasulu, Uvinza, Buhigwe, Kibondo, Kakonko na Kigoma.
Akizungumza kwenye Mkutano wa Baraza la Maalum la Madiwani kwa ajili ya kupokea na kupitia Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Wilayani Buhigwe, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amezipongeza Halmashauri hizo na kuzielekeza kujiwekea mikakati ya muda mrefu itakayolenga kupunguza hoja zisizokuwa za lazima.
Amesema Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali imebaini uwepo wa tatizo sugu la utunzaji sahihi wa nyaraka za kifedha zikiwemo zile za manunuzi pamoja na matumizi ya Masurufu.
‘’Yanapofanyika manunuzi na matumizi mengineyo ya masurufu, risiti zinazothibitisha matumizi yaliyofanyika ziwasilishwe mapema sehemu husika na aandaliwe mtu maaalum atakayeratibu na kusimamia zoezi la kuzipokea na kuzitunza ili zitakapohitajika ziweze kupatikana kwa urahisi’’ amesema.
‘’Nawaelekeza Wakurugenzi katika Halmashauri zote mkoani hapa kuanzisha Ofisi Maalum itakayotekeleza jukumu la utunzaji wa Nyaraka za Manunuzi katika Miradi inayotekelezwa na Serikali kwenye Halmashauri hizo. Tukifanaya hivyo itatusaidia kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa nyaraka muhimu kwa ajili ya kujibu hoja za ukaguzi’’ amesisitiza Andengenye.
Ameendelea kusema, Kitengo cha Manunuzi na Ugavi kimeendelea kuwa kinara kwenye kuzalisha hoja za ukaguzi ambapo amewataka wakuu wa vitengo hivyo kuhakikisha utendaji wao unazingatia Sheria na Kanuni za Manunuzi ili kuepuka kusababisha hoja ambazo kimsingi zinaweza kuzuilika.
Aidha Mkuu wa Mkoa amezitaka Menejimenti katika Halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma kuibua vyanzo vipya vya Mapato, kuimarisha vile vinavyoonekana kusuasua, kufuatilia utendaji kazi wa wakusanya mapato pamoja na mashine za kukusanyia mapato hayo.
‘’Nasisitiza fuatilieni na kubaini changamoto zilizopo kwenye zoezi zima la ukusanyaji wa mapato, mtakapobaini mashine zenye dosari ziondoeni kwenye mfumo na watendaji watakaobainika kufanya ubadhirifu wa Fedha za Makusanyo wachukuliwe hatua za kisheria’’ amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Upande wake Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Hesabu za Serikali CPA Honest Muya amesema pamoja na kupatikana kwa Hati hizo Safi kwa Halmashauri za Mkoa wa Kigoma, Menejimenti zinatakiwa kutoa ushirkiano mkubwa kwa wakaguzi wa ndani.
‘’Hoja huanza kuibuliwa na wakaguzi waliopo katika ngazi za Halmashauri na zinapokosa utatuzi, ndipo hufika ngazi ya mkaguzi wa nje, hivyo wakaguzi wa ndani wakipewa ushirikiano wa kutosha hoja nyingi zitaishia katika ngazi ya Halmashauri’’ ameshauri Muya.
Kuhusu kukabiliana na hoja za zamani, Muya amesema ni muhimu kila Halmashauri kuweka mikakati ya muda mrefu na yenye kuleta matokeo chanya ili kuhakikisha hoja hizo zinapunguzwa au kufutwa kabisa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa