Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 Sahili Geraruma, ametoa Rai kwa wakazi wilayani Buhigwe mkoani Kigoma kuendelea kutunza Mazingira kwa kupanda miti katika vyanzo vya Maji na pembezoni mwa Mto Malagarasi ili kuendelea kukitunza chanzo hicho kikuu cha Maji katika Ziwa Tanganyika.
Rai hiyo imetolewa leo Tarehe 1, Oktoba 2023 mara baada ya Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge kuzindua Mradi wa Kitalu cha Miti ya hifadhi ya Mazingira chenye Jumla ya Miche 1,031,000 unaotekelezwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya uhifadhi wa Mazingira, Bliss Green Generation katika kijiji cha Biharu kilichopo Kata ya Biharu wilayani Buhigwe mkoani hapa.
‘‘Maeneo mengi vyanzo vya Maji vinazidi kukumbwa na tishio la kukauka, hivyo miti hii ipandwe katika maeneo hayo na hakikisheni mnailinda ili lengo mlilolikusudia liweze kutimia’’ alisisitiza Geraruma.
Aidha Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge, amewataka wananchi kuepuka kufanya shughuli za kibinaadam katika maeneo yote ya vyanzo vya maji huku akisisitiza kuzingatia sheria za Serikali zilizowekwa kwa ajili ya Ulinzi na utunzaji wa vyanzo hivyo.
Naye Lukindo Hiza ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira linalofadhili Mradi huo kupitiaProgram ya Tuungane, amesema miche hiyo itagawiwa bure kwa wananchi wa maeneo hayo na yale ya jirani kwa lengo la uhifadhi wa bonde la mto Malagarasi.
‘‘Ifahamike kuwa, mto Malagarasi ndicho chanzo kikuu cha Ziwa Tanganyika, hivyo tusipotunza chanzo hicho tutapoteza urithi wetu wa asili ambao pia ni chanzo kimojawapo cha uchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma’’alisema Hiza.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Biharu, wameshukuru kuanzishwa kwa mradi huo kwa kueleza kuwa, miti hiyo itakapopandwa itaimarisha vyanzo vya maji, upatikanaji wa mvua na kupendezesha mazingira.
‘‘Miti hii itarudishia miti ya awali iliyowahi kuwepo katika maeneo yetu, hivyo itakapokua na kustawi itarejesha tabia ya nchi kama iliyokuwepo awali kabla ya uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanyika’’ alisema Eliudi Mbiliti.
Uzinduzi wa Kitalu hicho cha Miti umefanyika baada ya kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2022, kuzindua vyumba viwili vya madarasa Shule ya Sekondari Mnanila, mradi wa vijana (bodaboda) pamoja na kuweka jiwe la msingi Kituo cha Afya mwayaya ambapo miradi yote ina thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni mia sita.
Aidha Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, zimezindua Klabu ya wapinga Rushwa katika shule ya Sekondari Munanila pamoja na Klabu ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya katika Shule ya Msingi Milenda.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa