Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa yenye hali ya Hewa na Ardhi inayoruhusu uzalishaji wa mazao mbalimbali ya Chakula kinachoweza kutosheleza katika upatikananji wa mlo kamili na kusaidia kupunguza tatizo la utapiamlo katika Jamii.
Ukosefu au kutozingatia Elimu ya lishe bora kumeendelea kusababisha tatizo la udumavu kwa watoto, utapiamlo wa kadri na mkali, uwepo wa watoto wanaozaliwa na uzito pungufu na uwepo wa wanawake wajawazito wenye lishe duni.
Matokeo ya Utafiti wa Taifa wa Lishe uliofanyika Novemba 2018 umeonyesha uwepo wa udumavu kwa watoto walio chini ya miaka 5 kwa 42.3%, utapiamlo mkali 3.2%, utapiamlo wa kadri 4.7% watoto wanaozaliwa na uzito pungufu 5.6% na wanawake wajawazito wenye lishe duni 6.7%.
Utekelezaji wa Afua za lishe umeendelea kufanyika mkoani Kigoma ukiwa na lengo la kuijengea uwezo jamii na kuongeza ufahamu katika masuala ya Lishe na kupunguza utapiamlo wa aina zote.
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wadau wa maendeleo wanaotekeleza Afua za Lishe wameeendelea kuhamasisha ulishaji wa watoto, kupunguza upungufu wa madini mwilini, kuzuia vifo vya watoto vitokanavyo na utapiamlo mkali, kusimamia na kutekeleza mipango mbalimbali katika kuikabili changamoto ya lishe.
Kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2022 Afua za lishe zimetekelezwa mkoani Kigoma ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Elimu ya Lishe, matibabu ya watoto wenye utapiamlo, utoaji wa vidonge vya kuongeza wekundu wa damu, kupima na kudhibiti udumavu, usanisi na ulishaji watoto wenye umri wa miezi 0 hadi 23 na utoaji wa matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza.
Utekelezaji wa kazi hizo umeleta matokeo chanya katika jamii mbayo ni kushuka kwa kiwango cha watoto wanaozaliwa na uzito pungufu na kufikia 3.5% na 3.6% ya upungufu wa damu kwa wajawazito katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2022.
Serikali imeendelea na mkakati wa kupunguza tatizo la utapiamlo katika Mkoa kwa kutoa hamasa na elimu ya Lishe, uzalishaji na matumizi ya vyakula vinavojenga na kulinda mwili, Halmashauri zote kutenga shilling 1000 kwa mtoto ili kutekeleza shughuli za lishe na kuomba ufadhili katika kuendesha shughuli mbalimbali katika kuelimisha jamii kuhusu lishe bora.
Iwapo wakazi watazingatia Elimu ya lishe na kuitekeleza kwa vitendo, tatizo la udumavu, utapiamlo na maradhi mengine yatokanayo na lishe duni yatapungua mkoa Kigoma na kusababisha uwepo wa jamii yenye Afya bora.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa