Makamu wa Rais wa Jymhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia kwa Naibu wa Waziri wa Wizara hiyo Zainab Katimba kupitia upya Sheria Ndogo za Sekta ya Afya katrika Halmashauri zinazoruhusu kulipia kadi ya kliniki pamoja na kutoza faini kwa wanaojifungua nje ya vituo vya Afya ili kuzisitisha sheria hizo mara moja.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo Julai 12, 2024 akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Kasulu ambapo amepokea malalamiko ya wanawake kutozwa faini kati ya Shilingi 40,000 hadi Shilingi 50,000 na kusisitiza kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria na utaratibu huo unapaswa kusitishwa.
‘‘Changamoto hii inaonekana kuwepo maeneo mengi ndani na nje ya mkoa wa Kigoma hivyo ninaiagiza Wizara kupitia upya sheria hizo na kuandaa mwongozo wa kuziondoa kisha mzishushe kwenye Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji ili kuhakikisha utaratibu huo haujirudii tena’’amesisitiza Dkt. Mpango.
Amesema ni jukumu la watendaji wa serikali kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujifungua katika vituo vya Afya na inapotokea mjamzito kajifungua nje ya kituo cha kutolea huduma za Afya wahudumu wanapaswa kumpokea na kumpatia huduma bila masherti yoyote.
Akitolea ufafanuzi na maelekezo kero mbalimbali za wananchi zilizowasilishwa kupitia ziara hiyo, Makamu wa Rais amemuelekeza Afisa Biashara wa mji wa Kasulukuepuka kutumia nguvu wakati wa ukusanyaji wa makusanyo ya Halmashauri sambamba na halmashauri zote kutekeleza agizo la Serikali la kutotoza ushuru wa mazao kwa mzigo usiozidi tani moja.
Aidha ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuongeza kasi katika kushughulikia utoaji wa vitambulisho vya NIDA ili kutoa Fursa kwa wananchi kuvitumia kuendana na matakwa ya Serikali.
Sambaba na hayo, Makamu wa Rais ameuelekeza uongozi wa wilaya kupitia wakuu wa wilaya kuhakikisha wanatumia mbinu mbadala ili kuhakikisha ukosefu wa vitambulisho hivyo hauwanyimi fursa vijana kupata kazi katika mashirika au taasisi binafsi ili waweze kujipatia kipato.
Katika hatua nyingineDkt. Mpango ameuelekeza Uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA)kutekeleza jukumu lao la kutoa Elimu kwa Jamii badala ya kusumbua wamiliki wa vyombo vya Usafiri hususani waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda
‘‘Jukumu lenu la Msingi ni kutoa elimu na kuhamasisha watumiaji wa barabara wanazingatia taratibu na miongozo na wale watakaobainika kushindwa kuzingatia taratibu hizo ndio wachukuliwe hatua na sio kushinda mnakamata vyombo hivyo kabla ya kutoa elimu kwa Umma’’ alisisitiza Dkt. Mpango.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa