Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na uongozi wa Serikali ya Mkoa yamekuwa chachu ya kufikia malengo ya serikali kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Kigoma.
Mhe. Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo alipokutana na viongozi wa CCM na kusisitiza kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amekuwa kiunganishi kizuri baina ya pande mbili hizo kutokana na kufanya kazi kwa uwazi na ushirikishaji.
Amesema kumekuwa na ushirikiano mkubwa baina ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya CCM, jambo linalowapa fursa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu kazi zinazofanywa na kuendelea kuiamini serikali kupitia ushirikishwaji huo.
‘‘Nitoe pongezi zangu za dhati kwako Mkuu wa Mkoa kutokana na kushirikiana bega kwa bega na viongozi hao ambao ndio wawakilishi wa wananchi katika maeneo yao, jambo linalosababisha kuondoa migogoro na mivutano isiyo ya lazima katika usimamizi na utekelezaji wa kazi mbalimbali za miradi ya maendeleo mkoani hapa’’ amesema Makamu wa Rais.
Aidha Makamu wa Rais amewataka viongozi hao wa Chama Cha Mapinduzi kuwa wajumbe na mabalozi wazuri katika kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura sambamba na kujitokeza kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kupiga au kupigiwa kura ili nchi iweze kupata viongozi bora.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amepongeza uamuzi wa mkuu huyo wa mkoa kwa kwa kuruhusu wananchi wanaodaiwa kulima katika eneo la hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini mwanzoni mwa Mwaka huu, kuwataka kuondoa mazao yao bila kuzuiliwa na watendaji kutoka wakala wa Huduma za Misitu nchini(TFS).
‘‘Haiwezekani mtu analima mnamuacha, anapalilia mnamuangalia tu, wakati wa kuvuna ndipo mnaanza kupambana nae na kumnyang’anya mazao yake kwa kosa la kulima katika eneo la hifadhi, huo ni unyanyasaji mkubwa kwa nini msiwadhibiti wakulima hawa katika hatua za awali ili wasilime kabisa bali mnakuja kuwasumbua wakati wa kuvuna? Hili linafikirisha sana’’ amesema Dkt. Mpango.
Pamoja na hayo, Makamu wa Rais amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuendelea kuelekeza fedha nyingi mkoani Kigoma kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuboresha maisha ya wakazi mkoani Kigoma.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa