MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. PHILIP MPANGO AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI MUYAMA MARA BAADA YA KUSHUHUDIA MAPOKEZI YA MADARASA MATATU NA OFISI MBILI ZILIZOKARABATIWA NA BENKI YA TCB PAMOJA NA VIFAA VYA KITAALUMA IKIWEMO KOMPYUTA MOJA, MASHINE YA CHAPA PAMOJA NA MADAWATI 24. KUSHOTO KWAKE NI MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amehimiza Jamii kusimamia na kuipa kipaumbele Elimu ili kuboresha mifumo wa Maisha ya wakazi mkoani Kigoma.
Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa ziarani kwenye wilaya za Buhigwe na Kasulu mkoani hapa, Dkt. Mpango ameitaka jamii mkoani kuhakikisha watoto wote wanasoma bila kujali hali zao za kiafya au jinsia na kuhitimu kulingana na kiwango watakachotakiwa kukifikia kuendana na miongozo ya kitaaluma.
Amesema Serikali inaendelea kuweka Mazingira bora na rafiki kwa ajili ya ufundishaji na ujifunzaji, hivyo wazazi watumie fursa ya uwepo wa Miundombinu rafiki kwa utoaji na upatikanaji wa Taaluma, kuhakikisha watoto wanasoma na kufaulu ili waweze kujikomboa wao wenyewe na Taifa kwa ujumla.
Kiongozi huyo amewataka wazazi kutoruhusu wanafunzi kuolewa au kushiriki vitendo visivyo vya kimaadili hali itakayochangia kushindwa kuendelea na Masomo hivyo kutofikia malengo tarajiwa.
‘’Wanafunzi jukumu lenu kubwa ni kusoma kwa bidii ili muweze kupata maarifa mapya, jambo litakalowasaidia kufaulu na kuwavusha hatua nyingine katika Safari yenu ya Kitaaluma mpaka kufikia malengo mliyojiwekea’’ amesisitiza Mpango.
Pia Makamu wa Rais amewasisitiza walimu kuendelea kufundisha kwa bidii ili kuinua kiwango cha ufaulu mkoani Kigoma hali itakayoongeza idadi ya watalaam watakaolitumikia Taifa katika ngazi mbalimbali.
Katika kuongeza Motisha ya kitaaluma Shule ya Msingi Muyama ambayo kiongozi huyo alisoma kwa ngazi ya Elimu Msingi, Dkt. Mpango ameahidi kutoa Fedha kiasi cha Shilingi Mil. 3 kila Mwaka kwa wanafunzi watakaofanya vizuri kitaaluma pamoja na Mwalimu kinara wa ufundishaji.
‘’Nakuelekeza Mkuu wa Wilaya ukae na wataalam wa Idara ya Elimu Msingi ili muone namna bora ya kuanzisha Tuzo ambapo Mwanafunzi Bora Kitaaluma kati ya watakaohitimu Elimu ya Msingi atapata Shilingi Mil. 1, Mwanafunzi wa kike atakayefanya vizuri kitaaluma pia atapata Mil. 1 pamoja na Mwalimu ambaye somo lake wanafunzi watafanya vizuri’’ amesema Mpango.
Katika hatua nyingine Dkt. Mpango amewataka wakazi kujenga utamaduni wa kupanda miti rafiki kwa Mazingira ili kuhuisha vyanzo vya maji vilivyoathiriwa na uharibifu mkubwa wa Mazingira mkoani hapa.
Pia Makamu wa Rais amesisitiza upandaji wa miti ya matunda kwani mbali ya kutunza mazingira, itasaidia kuinua Uchumi wa wananchi kutokana na uuzaji wa matunda yatakayozalishwa.
Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa wakazi, kujenga Mazingira rafiki kwa wawekezaji wenye Dhamira ya kuwekeza mkoani Kigoma ikiwemo kukodisha au kuwauzia ardhi kwa kufuata utaratibu utakaokuwa na tija kwa pande zote mbili.
‘’Niwaase ndugu zangu, siku zote Maendeleo ya Mkoa wetu yataimarishwa na watu wenye nia ya kuwekeza na kutoa fursa za ajira kwa vijana wetu, hivyo mnatakiwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa wenye nia kama hiyo wanapowafikia jambo litakaloimarisha kiuchumi na kuendelea kuufungua’’ amesisitiza Dkt. Mpango.
MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE AKIZUNGUMZA NA WANAFUNZI PAMOJA NA WAKAZI WA MUYAMA (HAWAPO PICHANI)
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa