Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli ametoa wito kwa Jamii mkoani Kigoma kubadilika kutoka kwenye fikra na vitendo vyenye viashiria vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuimarisha Maadili na Upendo katika Familia na Jamii kwa Ujumla.
Kalli ametoa wito huo alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye Sherehe ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia ambapo kilele chake kimkoa kimefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Amesema Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo ya Amani Maadili na Upendo kwa Familia Imara, inatukumbusha wazazi na walezi umuhimu wa kusimamia maadili mema na upendo miongoni mwa wanafamilia kwa lengo la kujenga jamii yenye amani, upendo na Mshikamano.
Kupitia hotuba yake, Kalli amesema Maendeleo makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili katika Jamii kutokana na muingiliano mkubwa wa mila na desturi za kigeni katika mifumo ya kimaisha katika jamii.
‘’Matumizi ya mitandao ya kijamii, runinga pamoja na ufuasi mkubwa wa mitindo ya maisha ya kigeni, vimechangia kuhamasisha vitendo vya ngono, uhalifu wa kimitandao, msongo wa mawazo pamoja na kuingiza tamaduni zisizo na maadili mema kwa Taifa letu’’ amesema.
Ameendelea kusistiza kuwa, pamoja na Serikali kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti vitendo vunjifu vya maadili na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, bado kumekuwepo na matukio ya ukatili na unyanyasaji mkubwa dhidi ya kundi hilo.
‘’Kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2022, jumla ya matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yalikuwa 12,163, huku sababu kubwa zikitajwa kuwa ni uwepo wa Imani potofu, mila na desturi zenye madhara kwa makundi hayo, umasikini unaosababisha wazazi kushindwa kutekeleza majukumu yao kifamilia pamoja na uelewa duni wa masuala ya haki na Sheria’’ amefafanua Kalli.
Aidha, Kalli amewasihi wanajamii kuzingatia Sheria za nchi, kudumisha Amani na Upendo, huku akisistiza watendaji wa Serikali kuendelea kutoa Elimu na msaada wa kisheria dhidi ya wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji hususani wanawake na watoto.
Pia amewataka wataalam wa Serikali kutoka sehemu na vitengo vya Maendeleo na Ustawi wa Jamii, Elimu, Afya, Sheria na Dawati la Jinsia kuratibu na kutekeleza kwa ukamilifu Afua zote za kupambana na kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani hapa.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma amesema Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaosimamia haki za Wanawake na watoto katika Jamii wataendelea kujikita katika kutoa msaada wa kiushauri na namna ya kuvifikia vyombo vya Sheria ili kuhakikisha Jamii inaishi kwa haki, usawa na maelewano.
Mbwanji amesisitiza kuwa, iwapo watoto watapata malezi bora kutoka kwenye familia au jamii, itapunguza wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili na kukithiri kwa vitendo vilivyo kinyume na maadili katika jamii kwa siku za usoni.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa