Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Komredi Daniel Chongolo amewaasa Wananchi kuunga Mkono juhudi za Serikali katika kushirikiana na wawekezaji kwa lengo la kuimarisha Uchumi wa Taifa.
Chongolo ametoa wito huo alipozungumza na wakazi pamoja na wanachama wa CCM Mkoa wa Kigoma na Katavi katika Uwanja wa Community Centre mjini Kigoma, akiwa katika ziara yake ya kutoa Elimu kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Uwekezaji na Uendelezaji wa Bandari nchini.
Amesema Msimamo wa CCM ni kuweka Msukumo na kipaumbele katika kushirikiana na Sekta Binafsi hususani wawekezaji ili kuimarisha Uchumi kwa lengo la kuwaletea Maendeleo Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Ameendelea kufafanua kuwa, Serikali inatambua na haipo tayari kuingia Mkataba utakaolitia Hasara Taifa, bali dhamira ni kufanya maboresho makubwa katika uendeshaji wa Sekta hiyo ili iweze kuleta manufaa kiuchumi
‘’Mivutano mnayoendelea kuishuhudia na hoja zinazoendelea kujengwa na makundi mbalimbali kuhusu Mkataba huu zinatokana na vita ya kugombea fursa za kiuchumi dhidi ya mataifa ambayo tutaingia nayo ushindani wa kibiashara kupitia uwekezaji tunaoenda kuufanya’’ amefafanua.
‘’Niwahakikishie kuwa uwekezaji unaoenda kufanywa na Serikali sio tu utaimarisha Bandari ya Dar es Salaam tu bali hata zile zilizopo mikoani na kutoa fursa ya ajira pamoja na kuimarisha utoaji wa Huduma kwa Wateja kwenye Maeneo hayo’’ amesisitiza Chongolo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amesema Dhamira ya Serikali kwenye uwekezaji wa Bandari inalenga kuongeza uwezo wa kushughulikia mizigo ili iwahi kuwafikia walengwa na kutoa fursa ya kuhudumia Idadi kubwa ya wateja kwa muda mfupi, hali itakayosaidia kuongeza mapato ya ndani ya nchi.
Dkt. Mkumbo ameeleza ‘’Serikali ilifanya utafiti wa kina wenye lengo la kubaini Kampuni yenye uwezo mkubwa katika kutoa Huduma za Bandari kwa kuzingatia uzoefu, utendaji kazi mzuri pamoja na tija kwa Taifa hadi kufikia maamuzi ya kumpata mwekezaji.
Amefafanua kuwa Lengo ni kuongeza uwezo katika kuzihudumia nchi zinazotumia Bandari ya Tanzania zikiwemo Zambia, Congo, Burundi, Rwanda na Uganda ili kutoruhusu uwezekano wa kupokea mizigo kupitia Bandari za nje hali itakayosababisha tupoteze fursa hiyo muhimu ya kujiimarisha kiuchumi.
‘’Rais wetu ni mpenda haki na ameruhusu Demokrasia hali inayotoa mwanya kwa watu kuchangia mawazo yao na hata kukosoa bali, mtambue lengo kuu la Serikali ni kutumia uwekezaji kama njia bora ya kuimarisha uchumi’’ amesisitiza Dkt. Kitila Mkumbo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete (Mb) amesema suala la uwekezaji bandarini ni la muda mrefu na maamuzi ya Serikali kubadilisha Mwekezaji yametokana na kuwepo kwa uendeshaji usio na Tija katika eneo hilo.
‘’Reli zetu zinauwezo wa kusafirisha mizigo hadi kufikia zaidi ya Tani Mil. 30 kwa Mwaka ambapo kwa sasa uwezo wetu ni tani Mil. 23, jambo linalolalamikiwa na wateja kutokana na mizigo mingi kushindwa kutoka kwa wakati bandarini na kuwasababishia hasara wafanyabiashara’’ amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema maboresho makubwa ya Miundombinu ya Uchukuzi na Usafirishaji mkoani Kigoma yatakuwa chachu katika kuongeza Ufanisi wa kibiashara mara baada ya uwekezaji huo muhimu katika Bandari kukamilika.
Amesema kwa kuwa mkoa unapakana na nchi jirani za Burundi na Congo uwekezaji huo utakapokamilika utatimiza dhamira ya Mhe. Rais Samia ya kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa kitovu Biashara na Uchumi kwa ukanda wa Magharibi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa