MKUU WA MKOA WA KIGOMA KAMISHNA JENERALI MSTAAFU WA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI MHE. THOBIAS ANDENGENYE AKIPOKEA TUZO YA KUTAMBUA UTENDAJI KAZI WAKE MZURI KUTOKA JUMUIA YA KIKRISTO TANZANIA (CCT) MKOA WA KIGOMA ILIYOKABIDHIWA NA BABA ASKOFU OSWARD BAVUMA AMBAYE NI MWENYEKITI WA JUMUIA HIYO MKOANI KIGOMA MEI 27,2024.
Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Kigoma imekabidhi Tuzo Maalum ya kutambua kazi nzuri inayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma katika kuhahakisha wananchi wanapata Maendeleo pamoja na kusimamia amani, umoja na mshikamano kwa wakazi mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Mkoa, ameushukuru uongozi huo wa CCT na kuahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa madhehebu ya dini mkoani hapa kwa lengo la kuimarisha Amani na mshikamano kwani ndio msingi wa Maendeleo.
Amesema viongozi wa dini wananafasi kubwa ya kuzungumza na wananchi hivyo kupitia mahubiri yao wanapaswa kuendelea kuhamasisha na kuikumbusha jamii umuhimu wa kujenga familia zenye kuheshimu misingi ya Imani za kidini ili kuimarisha malezi yenye maadili kwa watoto.
Aidha Andengenye ameitaka Jamii mkoani hapa kuendelea kujiimarisha katika Imani za kidini kwa lengo la kumtumikia Mungu na kuachana na Imani za kishirikina jambo linaloleta mifarakano na uvunjifu wa Amani.
Upande wake Mwenyekiti wa Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Kigoma Askofu Osward Bavuma amesema zawadi iliyotolewa kwa mkuu wa mkoa ni salamu ya upendo kutoka kwa waumini walio chini ya umoja huo, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Jumuia ya kikristo Tanzania.
Kupitia salamu za jumuia hiyo, Askofu Bavuma amesema pamoja na mambo mengine, Jumuia hiyo inatekeleza kazi za utoaji wa huduma za kimalezi kwa vijana waliopo ngazi mbalimbali za kimasomo pamoja na kutoa misaada kwa watoto wanaoishi Mazingira hatarishi.
Sambamba na hayo, ameitaja changamoto ya uwepo wa Imani za kishirikina miongoni mwa wakazi hususani kuibuka kwa wimbi la wapiga ramli chonganishi maarufu Kamchape kuwa ni janga la kiimani mkoani hapa.
Amesema, wananchi wanapaswa kubadilika na kuachana na Imani za kishirikina kwani zimekwisha sababisha athari kwa baadhi ya wakazi ikiwemo uharibifu wa mali, watu kujeruhiwa na baadhi ya wakazi kuyakimbia makazi yao.
Amesisitiza kuwa, uongozi wa CCT utaendelea kuunga mkono kazi nzuri zinazoendelea kutekelezwa na serikali ya awamu ya sita mkoani hapa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kwa kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, yameshuhudiwa na mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye maadhimisho ya Siku ya Jumuia ya Kikristo kimkoa yaliyofanyika Mei 26, 2014 mkoani hapa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa