Mradi wa Binti (Binti Project) umetajwa kuwa mkombozi katika kuhakikisha watoto wa kike katika vyuo vya ufundi mkoani Kigoma wanatimiza ndoto zao kwa kuimarisha Afya ya Hedhi salama.
Akizungumza alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye uzinduzi wa Mradi huo sambamba na kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama duniani, Dkt. Albert Mwesiga amesema walezi na Jamii kwa ujumla wanapaswa kuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika kuimarisha huduma za hedhi salama mkoani Kigoma.
Amesema mradi wa Binti unalenga kutoa elimu ya Afya kuhusu hedhi salama, uimarishwaji wa miundombinu kwenye vyuo vya ufundi sambamba na ugawaji sodo kwa wananfunzi wa kike katika vyuo vya ufundi.
Aidha kupitia mradi huo, matarajio ni kuviwezesha vikundi vya akina mama wajasiriamali kupata mafunzo ya ushonaji wa taulo za kike sambamba na kuwapatia mashine za kushonea taulo hizo ambazo ni salama Zaidi kwa afya za watumiaji.
Aidha ametoa rai kwa wanufaika wote wa mradi huo wakiwemo wanafunzi wa vyuo vya ufundi na vikundi vya akina mama kuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika kuimarisha huduma za hedhi salama kwenye Jamii.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la (AfriCraft) linaloratibu upatikanaji wa Sodo na utoaji wa Elimu kuhusu hedhi salama AfriCraft Kelvin Nicholaus amesema vyuo vya ufundi vimekuwa havipewi kipaombele katika utoaji elimu ya Hedhi salama jambo ambalo limelisukuma shirika hilo kutoa elimu na huduma ya uboreshaji wa taulo za kike kwa wanachuo mkoani hapa.
Amesema kuwa mradi huo umezinduliwa mkoani kigoma na utaendelea katika mikoa mingine sita 6 iliyobakia ili kuwawezesha kupata taulo kwa matumizi zaidi ya mara Moja na kutoa elimu juu ya utengenezaji wa taulo hizi za kike kwa kipindi cha miaka miwili 2024/2026.
“Tumezingatia madhara anayoweza kupata mtoto wa kike na kutengeneza sodo hizi ambazo zitamuwezesha kuwa huru na kuweza kuyatimiza majukumu yake wakati anapokuwa kwenye hedhi bila kupata maambukizi ya magonjwa sambamba na kuaibika kwa kukosa sodo za kutumia wakati awapo hedhi” amesema Nicholaus.
Mradi huo ulianza mwaka 2020 na kwa sasa unatarajia kuwafikia zaidi ya wanafunzi wa kike 12,000 pamoja na Vyuo 15 vya ufundi katika mikoa ya Tanga ,Kigoma, Dar es salaam, Morogoro, Rukwa, Lindi na Zanzibar.
Ameongeza kwa kusema kuwa shirika la Africraft linaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na ya serikali katika kuboresha suala la hedhi salama na upatikanaji wake kwa watoto wa kike.
Kwa upande wake Mwanachuo kutoka Chuo cha Kigoma Training College, Jackline Matias ameishukuru serikali kwa kushirikiana na wadau kwa kuligusa kundi hilo kwa sababu kwa kuwawezesha kupata taulo bure na kuwaweka huru katika shuguli mbalimbali zikiwemo za kimichezo.
Maadhimisho hayo yameambatana na Kauli mbiu isemayo “Pamoja kwa Hedhi Rafiki Ulimwenguni “huku kauli mbiu ya Mradi ikiwa ni ‘’Uwezeshwaji wa msichana kupitia Hedhi salama”.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa