Jamii mkoani Kigoma imeaswa kuendelea kuwatunza na kuwajali wazee na watu wengine wenye mahitaji maalum badala ya kuiachia Serikali na Taasisi za kiraia.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi Bima za Afya kwa wazee zilizotolewa na Taasisi ya Endeleza Wazee Kigoma (EWAKI), Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Ntime Mwalyambi amesema jukumu la kuwatunza na kuboresha maisha ya wazee pamoja na watu wenye mahitaji maalum, lisiachwe mikononi mwa Serikali na Taasisi binafsi bali kila mtu atambue anao wajibu wa kulitazama na kulitunza kundi hilo muhimu kwa ustawi wa Taifa.
‘’Wazee ni tunu ya Taifa na ndiyo waliotufikisha hapa tulipo hivyo ni jukumu la kila mmoja kuguswa na uwepo wa kundi hilo bila kusukumwa katika kutoa huduma hitajika na kuwafanya waendelee kufurahia uwepo wao’’ amesema Mwalyambi.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa EWAKI Bi. Clotilda Kokupima amesema kupitia utafiti walioufanya wamebaini hitaji la Matibabu ni changamoto inayoongoza katika mahitaji miongoni mwa wazee wengi mkoani Kigoma.
Kokupima amefafanua ‘’ tumedodosa masuala mbalimbali ikiwemo Usalama, hitaji la chakula, mavazi, usafi, nk, lakini tumeona kipaumbele ni suala la Afya, wazee wengi wanashindwa kumudu gharama za matibabu’’
Afisa Tawala wa Taasisi ya EWAKI Costa Alfred amesema kwa mwaka 2023, Taasisi hiyo imetoa Jumla ya Bima za Afya 400 zenyeThamani ya Shilingi Mil. 3 kwa ajili ya wanufaika 2400 ambao ni wazee pamoja na wategemezi wao.
Ameendelea kufafanua kuwa, mpango wa utoaji wa Bima hizo ni endelevu na utaendelea kutekelezwa kwa kipindi cha Miaka Miwili ambapo kwa Mwaka 2024 matarajio ni kutoa Bima kwa wanufaika 2400 ili kufikisha lengo walilojiwekea la kutoa Bima kwa wanufaika 4800.
Upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Anna Akyoo ameishukuru Taasisi hiyo na kutoa wito kwa Taasisi nyingine za Kiraia kusaidia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kundi hilo.
‘’Awali nitoe Shukurani kwa Taasisi ya EWAKI, lakini niziombe Taasisis nyingine mkoani hapa kusaidida katika kukabili changamoto zinazowakabili wazee wetu mkoani Kigoma ili waweze kuishi kwa furaha na amani’’ amesisitiza Akyoo.
Baadhi ya wazee walioshiriki Hafla hiyo hawakusita kutoa Shukurani zao huku wakiiomba Serikali, Wadau pamoja na Jamii kwa ujumla kutowasahau huku wakisisitiza kuwa wao ndio waasisi wa Taifa na Maendeleo yaliyopo leo wamehusika kwa kiasi kikubwa kuhakikisha yanafikiwa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa