Zaidi ya Sh. 5.78 bilioni zimeidhinishwa kutumika katika ujenzi wa madaraja na ukarabati wa Barabara chini ya wakala wa Barabara Mjini na vijijini (Tarura) Mkoani hapa.
Kiasi hicho cha Fedha kitatolewa mara baada ya Serikali kusaini Mikataba 18 na Makandarasi wanaotarajiwa kuanza kufanya utekelezaji wa kazi hizo katika Halmashauri nane za Mkoa wa Kigoma kwa mwaka wa Fedha 2022/2023.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kabla ya utiaji saini mikataba hiyo, Kanali Michael Ngayalina ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, aliwataka Makandarasi kutekeleza Miradi hiyo kwa kuzingatia muda wa mkataba pamoja na miongozo ya utendaji wa kazi inayotolewa na Serikali ili kufanya kazi zenye ubora na kuwaharakishia wananchi maendeleo.
‘’Barabara ni kiungo muhimu kwa Maendeleo ya wananchi kwani mbali ya kurahisisha mawasiliano, inarahisisha ukuaji wa uchumi wa Taifa kutokana na kuruhusu usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za kibiashara’’ alisema.
‘’Serikali imewaamini nanyi mkatekeleze kazi hizo kwa uadilifu huku mkitanguliza uzalendo badala ya kujali maslahi binafsi na kufanya kazi mlizopewa kwa kiwango cha chini ili mpate faida kubwa.’’ alisistiza Kamali Ngayanila.
Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Kigoma, Senzia Maeda, alisema jumla ya kazi 20 za matengenezo ya barabara na ujenzi wa madaraja zilitangazwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa Halmashauri za Mji Kigoma-Ujiji na Kasulu pamoja na wilaya za Kigoma vijijini, Uvinza, Kasulu, Buhigwe, Kibondo na Kakonko ambapo kazi 19 zilipata makandarasi na moja kukosa kwa kutokidhi vigezo vya zabuni.
‘’ Mikataba iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo ina Thamani ya Shilingi 5, 784,699,286.00 na tunatarajia mara baada ya zoezi hili la kusaini mikataba, kazi zitaanza ndani ya muda mfupi ili kuwaondolea kero na adha ya usafiri wananchi katika maeneo yatakayoguswa na utekelezaji huo’’ alisema Maeda.
Naye Mkandarasi Dalali Abdallah, alisema anaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaamini Makandarasi wazawa katika utekelezaji miradi hiyo huku akiahidi kutekeleza kazi hiyo kwa uadilifu na uaminifu.
‘’Tutajitahidi kufanya kazi kwa kuzingatia muda na miongozo ya Serikali pia kuhakikisha kazi tunazofanya zinakuwa kwenye kiwango bora kwa kuwa tunafanya kazi hizi kwa maslahi yetu tukiwa watanzani’’ alisema Dalili.
Kazi zitakazofanyika kupitia Zabuni hizo ni uboreshaji wa barabara kwa kiwango cha lami jumla ya Kilomita nane pamoja na kiwango cha Changalawe kwa zaidi ya Kilomita mia nne ikiwa ni barabara mbalimbali katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Kigoma.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa