Jumla ya Shilingi billion 32 kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF zimetumika katika miradi mbalimbali katika kupuguza umasikini Mkoani Kigoma, ikiwemo kuziwezesha kaya Masikini.
Haya yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Emanuel Maganga leo amekutana na kufanya Mazungumzo na mwakilishi wa wahisani wa Mfuko wa Maendelo ya Jamii TASAF ambaye pia ni mshauri wa masuala ya uchumi katika Ubalozi wa Sweeden hapa nchi Bi. True Schedvin.
Akitoa shukrani zake kwa wahisani Maganga amesema anawashukuru kwa moyo wao wa kujitoa kusaidia kupunguza umaskini katika Mkoa wa Kigoma. “Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma tunafarijika na moyo wenu wa kusaidia jitihada za kuondoa umaskini kwa wananchi, tunatambua wazi fedha mnazotoa si ziada kwenu bali ni matashi mema ya kutaka wananchi wetu hapa Kigoma waondokane na umaskini” aliongeza Maganga.
Mhe. Maganga amemhakikishia Bi. Schedvin kuwa Serikali ya Mkoa wa Kigoma itahakikisha fedha zinazotolewa na wahisani zinasimamiwa kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi wa Kigoma na si vinginevyo.
Naye Bi. Schedvin amesema kuwa lengo la ziara yao ni kuangalia, utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Mfuko wa Maedeleo ya Jamii pamoja na changamoto zinazojitokeza ili kuweza kuzirekebisha.
Aidha watendaji wamehimizwa kusimamia kwa ukamilifu matumizi sahihi ya fedha za wahisani katika miradi mbalimbali kwa lengo la kubadili maisha ya wananchi wa Kigoma kuondokana na Umaskini.