Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Kigoma kutarahisisha upatikanaji wa Huduma bobezi za kiafya sambamba na kuongeza idadi ya watoa huduma za Afya mkoani Kigoma
Andengenye amesema hayo alipozungumza kwenye hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Majengo ya Chuo hicho Kampasi ya Kigoma na kusisitiza kuwa kukamilika kwa miundombinu hiyo kutatoa fursa kwa wataalam wa Afya mkoani Kigoma kupata mafunzo kwa vitendo na kuongeza ujuzi katika utoaji huduma za Afya.
Akiwasilisha taarifa ya hatua za utekelezaji wa mradi huo, Naibu Mratibu wa Mradi Dkt. Nathanael Sirili amesema kazi hiyo inatekelezwa kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) kwa Thamani ya Shilingi 26,088,071,158.84 ukitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2026 ambapo na kutekelezwa na Mkandarasi China Jianxi International Co. Ltd.
Dkt. Sirili amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa jengo la utawala, ukumbi wa mihadhara, maabara moja ya kompyuta, maabara sita za kufundishia na nyingine moja ya anatomia, ukumbi mkubwa wa mikutano, bweni la wanafunzi, bwalo la chakula, uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu pamoja na barabara za kuunganisha miundombinu itakayojengwa.
Amesema Historia ya Chuo Kikuu cha Muhimbili inaanzia mwaka 1963 kama shule ya udaktari ambapo mpaka kufikia mwaka 2024 kinatoa programu za mafunzo mbalimbali ya kiafya zipatazo 101 kwa ngazi za Shahada, stashahada, uzamili na uzamivu.
Amesema ni dhamira ya Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuimarisha mifumo ya utoaji wa Elimu ya Afya nchini ambapo kupitia Programu ya Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) Chuo kinatekeleza kazi za kuboresha miundombinu katika Kampasi ya Mloganzila na Kigoma.
Ameedelea kufafanua kuwa hadi kufikia Novemba 15, 2024, utekelezaji wa Mradi katika Kampasi ya Chuo hicho mkoani Kigoma ni pamoja na kupatikana kwa ardhi yenye ukubwa wa Hekta 19.1, kuandaa moango kazi wa matumizi ya eneo, kuandaa itifaki ya uanzishwaji wa eneo hilo sambamba na kuanza kwa usafi.
Amesema katika ujenzi utakaofanyika, jengo la utawala litakuwa na ofisi za watumiaji sitini, ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kutumika na watumiaji 50, ukumbi mkubwa wa mikutani watumiaji 300, maabara sita za kufundishia zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi sitini kila moja, maabara ya atomia yenye meza 29, bweni la wanafunzi 111, bwalo la chakula lenye uwezo wa kutumika na watumiaji 120 sambamba na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa kisasa.
Aidha miundombinu hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kupokea kwa hatua za awali jumla ya wanafunzi 300 kwa mwaka wa kwanza na kadri inavyoendelea itaweza kupokea jumla ya wanafunzi 5,673.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa