Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amemtaka Mkandarasi anayejenga barabara ya Kasulu Manyovu kwa Kiwango cha Lami kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ifikapo Machi 2025.
Akizungumza na maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Buhigwe akiwa katika Siku ya Pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma, Mhe. Dkt. Mpango amesema maendeleo yam Mkoa wa Kigoma yamechelewa kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu bora ya Barabara Maji, Umeme na Huduma nyingine za jamii kwa muda mrefu na kuwataka wananchi kutumia fursa ya kukamilika kwa miundombinu hiyo kujiletea Maendeleo.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo ambayo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Km 260.6 kutauunganisha mkoa wa Kigoma na Kagera pamoja na nchi jirani ya Burundi na kutoa fursa za kiuchumi kupitia usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za kibiashara.
Akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Buhigwe kwa nyakati tofauti tofauti, Dkt. Mpango amesema serikali inalenga kuimarisha miundombinu mbalimbali mkoani hapa ili kuufanya mkoa kuwa kitovu cha biashara na uchumi kwa ukanda wa Magharibi.
Aidha Makamu wa Rais, amewataka watendaji wa Serikali mkoani hapa kutumia muda mwingi katika kutembelea na kusimamia miradi ya Maendeleo pamoja na kutosita kuchukua hatua dhidi ya watendaji wazembe wanaochelewesha utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Upande wake Waziri wa Ujenzi Inocent Bashungwa amesema kwa kushirikiana na wasaidizi wake watahakikisha agizo la Makamu wa Rais linatekelezwa kama ilivyopangwa sambamba na miradi mingine ambayo ameelekeza wizara hiyo kufuatilia na kusimamia utekelezaji wake ili iweze kukamilika na kuwaondolea kero wananchi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa