Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso (Mb). Amefanya kikao Kazi kazi, ambapo amekutana na Wakuu wa Idara na Vitengo vilivyopo chini ya Wizara na kuwaagiza kuhakikisha Miradi ya Maji inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa huku akisisistiza kuwa, hatosita kuchukua hatua pale atakapobaini uzembe katika utendaji kazi.
Kupitia Kikao hicho kilichofanyika mkoani hapa, Waziri Aweso amesema maeneo mengi nchini miradi ya Maji inashindwa kukamilishwa kwa sababu zilizo ndani ya Mamlaka za kiutendaji huku Serikali ikiwa imeshapanga Bajeti na kupeleka Fedha katika maeneo hayo.
Amewaasa watumishi wa Wizara hiyo wabadilike kiutendandaji na kufanya kazi kwa ushirikiano huku akisisitiza Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuboresha utendaji kazi wao kutokana na uwepo na malalamiko mengi katika maeneo ya vijijini.
Amesema wakazi wa Mkoa wa Kigoma wanapaswa kupata huduma ya Maji kwa utoshelevu kutokana na uwepo wa ziwa Tanganyika, ambalo linaweza tumika kama chanzo cha uhakika cha upatikanaji wa huduma hiyo.
Awali Katika salamu zake za ukaribisho kwa Waziri wa Maji, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye, amesema changamoto kubwa ya ufanisi katika miradi ya Maji mkoani Kigoma ni ukosefu wa Umeme wa kutosha hali inayotatiza usambazaji wa huduma hiyo kwa Wananchi.
Aidha amesisitiza wananchi kutunza miradi ya Maji kwa kufanyia ukarabati dosari zitakazojitokeza badala ya kusubiri Serikali ili kuruhusu Bajeti iliyopangwa kutekeleza miradi mingine kwenye maeneo yenye uhitaji.
Kwa upande wao baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Kigoma, wamemshukuru Waziri kwa utendaji kazi wake huku wakishauri Wizara hiyo ione namna bora ya kutumia fursa ya uwepo wa vyanzo vya Maji vya Ziwa Tanganyika na Mto Malagarasi katika kutatua changamoto za huduma ya Maji mkoani hapa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa