WAZIRI WA MAJI MHE. JUMA AWESO (KATIKATI) AKIWA KATIKA KIKAO CHA WADAU WA MAJI MANISPAA YA KIGOMA UJIJI. KULIA KWAKE NI MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE NA KUSHOTO NI KATIBU TAWALA MKOA WA KIGOMA MHE. ALBERT MSOVELA.
Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso (Mb) amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha na kuimarisha Miundombinu ya Maji nchini ili kuwaondolea wananchi adha zitokanazo na changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo.
Waziri Aweso amesema hayo alipozungumza kwenye kikao cha pamoja kilichomkutanisha na wadau wa Maji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Hapa.
Waziri Aweso amesema pamoja na kuendelea kuimarika kwa upatikanaji wa Huduma hiyo Mkoani Kigoma, Serikali itaendelea kuhakikisha Maji yanayopatikana ni Safi, toshelevu na yenye ubora unaostahili kwa matumizi ya binadamu.
Amefafanua kuwa, Serikali inaendelea na Mchakato wa kuhakikisha Ziwa Tanganyika linakuwa chanzo kikuu na cha uhakika cha uzalishaji wa Maji yatakayotumiwa na wakazi katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi.
Aweso ametoa wito kwa wadau wa Maendeleo wanaotaka kuwekeza mjini Kigoma kutekeleza adhma hiyo ya kimaendeleo kutokana na utoshelevu wa Maji ambapo kwa sasa uzalishaji umefikia kiasi cha Lita Mil. 42 huku mahitaji halisi yakiwa ni lita Mil. 23.
Pia Waziri ameielekeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji kutokuwa kikwazo katika zoezi la usambazaji na utoaji wa huduma nyinginezo zinazohusu Maji kwa lengo la kusogeza na kuongeza hali ya utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa KigomaThobias Andengenye amesema Jumla ya Vijiji 306 vimepatiwa huduma ya Maji huku vingine 40 vikiwa havijafikiwa kabisa huku upatikanaji wa huduma hiyo ukipanda kutoka Asilimia 56 hadi kufikia Asilimia 67.3.
‘’Katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi ya Maji 49 katika vijiji 77 ambayo inatarajia kukamilika 2025 na kusababisha ongezeko la Asilimia 17.8 ya upatiakaji wa Maji mkoani hapa’’ amesema.
Ameendelea kusema kuwa, kazi mbalimbali zimeendelea kufanyika ikiwemo kutoa Elimu na kuhamasisha utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya maji kwa kuhamasisha upandaji wa miti rafiki kwa Mazingira.
Upande wake Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (KUWASA) Manispaa ya Kigoma Ujiji Poas Kilangi, amemueleza Waziri kuwa, katika Manispaa ya Kigoma Ujiji yenye kata 19 ikiwa na wateja hai wa Huduma hiyo 17, 347, mtandao wa Maji umefikia Km. 405.
Amezitaja chanagamoto zinazowakabili kiutendaji ikiwemo uchakavu wa Jengo la Ofisi, uhaba wa watumishi pamoja na kutotosheleza kwa vitendea kazi ikiwemo uhaba wa vyombo vya Usafiri.
Pia ameutaja udogo na uchakavu wa mabomba kuchangia kwa kiasi kikubwa kutopatikana kwa huduma ya uhakika ya maji katika baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Aidha katika kudhibiti matumizi ya holela ya Maji, Kilangi amesema wamefanikiwa kuagiza mita za Maji 2500 na wanaendelea kuzifunga kwa wateja ili kila mtu achangie huduma hiyo kuendana na matumizi yake.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa