Wananchi wanaoishi katika vijiji vya Mwambao wa Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi ya kuambukiza ikiwemo maradhi ya tumbo kutokana na baadhi ya wakazi kutokuwa na vyoo.
Akizungumza na wakazi wa kata ya Mwakizega wilayani Uvinza mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameagiza ujenzi wa kambi zote za Uvuvi katika maeneo hayo kufanyika sambamba na ujenzi wa vyoo ili kuepusha athari za kiafya kwa watumiaji wa Maji ya ziwa hilo.
‘’Nitumie fursa hii kuitaka jamii hususani wanaojishughulisha na uvuvi kuhakikisha wanajaenga vyoo kabla ya kuweka makazi pembezoni mwa ziwa, hii itatuepushia changamoto za maradhi ya mlipuko ikiwemo kipindupindu, na maradhi mengineyo ya tumbo’’amesema Andengenye.
Ameitaka jamii kuendeleza utaratibu wa kunawa mikono mara kwa mara, kuchemsha Maji kabla ya kunywa pamoja na kula vyakula vilivyoandaliwa na kuhifadhiwa katika hali ya usafi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakazi mkoani hapa kutumia miundombinu ya kielimu inayoendelea kuimarishwa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha watoto wanafikia malengo ya kitaaluma yaliyowekwa kuendana na miongozo ya Serikali.
‘’Hakikisheni watoto waliofikia umri wa kusoma, wanaandikishwa Shuleni na wazazi washirikiane na walimu katika kuwasimamia ili wamalize kwani kutokufanya hivyo ni kuwanyima watoto haki yao muhimu ya kitaaluma’’ amesisitiza.
Aidha Andengenye ameitaka Jamii kujenga utamaduni wa kupima Afya mara kwa mara badala ya kusubiri hadi kupatwa au kuzidiwa na maradhi.
‘’Tuondokane na dhana ya kuamini Vituo vya kutolea huduma za Afya ni sehemu ya matibabu pekee bali tutambue jukumu lao la msingi la kuchunguza maendeleo ya Afya zetu bila hata kuugua kwa sababu yapo maradhi yanaweza kuletha athari kwenye mwili bila kuonesha dalili katika kipindi kifupi’’ ameshauri Mkuu huyo wa Mkoa
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa