Jamii imeshauriwa kutumia mbinu na Maarifa mapya pamoja na kujiimarisha katika matumizi ya Teknolojia ili kuongeza tija katika uzalishaji mali na kujiletea Maendeleo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza kwenye kilele cha Maonyesho ya Sikukuu ya wakulima nane nane kanda ya Magharibi yaliyofanyika Mkoani Tabora.
Amesema jamii inapaswa kutumia zana za kisasa katika kuendesha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo matumizi ya Mashine pamoja na kujiimarishia maarifa kiutendaji , ili kuongeza kiwango cha uzalishaji pamoja na kupandisha thamani ya bidhaa zitakazozalishwa .
Ameeleza kuwa serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kukuza Sekta ya Kilimo , Mifugo na Uvuvi kwa kuanzisha majukwaa ya uwekezaji , kuongeza Bajeti za Wizara hizo pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati kwenye nyanja za kiuchumi kwa lengo la kuzidi kuifunga Kanda ya Magharibi.
‘Nimefurahishwa na uwepo wa ongezeko la Idadi ya vikundi vinavyojihusisha na uboreshaji wa Mnyororo wa Thamani kwa Mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hivyo msisiste kutumia fursa ya uwepo wa Masoko ya ndani na nje ya nchi kujinufaisha na kujiimarisha kiuchumi ’ amesisitiza Andengenye.
Aidha kiongozi huyo ametoa Rai kwa wakulima kuepuka hasara kwa kuendelea kuviamini na kuvitumia vyama vya Ushirika (AMCOS) kuuza mazao kwa bei zenye tija ili kufikia malengo ya kimaendeleo waliyojiwekea.
Kadhalika Andengenye amezipongeza Taasisi pamoja na watu binafsi waliojitokeza na kushiriki katika maonyesho hayo na kuwahimiza kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili kukuza sekta za Kilimo, Mifugo na uvuvi ndani na nje ya Mikoa ya Tabora na Kigoma.
Kilele cha maadhimisho hayo kimefanyika katika viwanja vya ipuli Manispaa yaTtabora na kuhudhuriwa na kaimu Mkuu wa Mkoa Tabora Peter Serukamba, Mwenyekiti wa CCM (M) Tabora , Makatibu Tawala (M) Tabora na Kigoma , Wakuu wa wilaya , wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya Tabora na Kigoma, wawakilishi wa wizara za kilimo, mifugo na uvuvi , watendaji kutoka Ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya Kanda ya Magharibi, Sekta binafsi, wakulima pamoja na wajasiriamali mbalimbali katika mikoa hiyo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa