MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE AKIPANDA MTI KUASHIRIA UZINDUZI WA MRADI WA UBORESHAJI WA USTAHIMILIVU WA TABIA YA NCHI MEI 6, 2023 KATIKA VIWANJA VYA OFISI YA MKUU WA MKOA WA KIGOMA.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema Serikali mkoani hapa inatambua athari hasi zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na iko tayari kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na wafadhili katika kukabiliana na kudhibiti hali hiyo.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo alipozungumza wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji Ustahilmilivu wa Tabia ya Nchi unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika wilaya zinazohifadhi wakimbizi mkoani Kigoma chini ya Mradi wa Pamoja wa Kigoma(Kigoma Joint Programme), Awamu ya Pili.
Amesema Uongozi wa Mkoa unafahamu Madhara yanayoletwa na mabadiliko ya hali ya Hewa na umeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuikabili hali hiyo ikiwemo kutekeleza agizo la Serikali la upandaji wa Miti pamoja na kuhamasisha wananchi kupunguza matumizi ya Nishati ya kuni na Mkaa.
‘’Nafahamu mradi huu utatekelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika ya kuhudumia wakimbizi pamoja na vitengo mbalimbali vilivyopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, nasisitiza mkatetekeleze kazi zenu kwa weledi na ubora ili kile kilicholengwa kiweze kufikiwa’’ amesisitiza.
‘’Huu ni mradi wa kwanza katika Awamu ya Pili ya Mradi wa Pamoja wa Kigoma, ambao umelenga kushirikisha Mashirika mbalimbali yanayohudumia wakimbizi kwa lengo la kusaidia kutatua changamoto mbalimbali kwa Jamii ambazo zinahifadhi wakimbizi katika baadhi ya Wilaya zetu mkoani hapa’’ Amesema Andengenye.
Upande wake Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania Mahoua Parums amesema hadi sasa nchi ya Tanzania inaendelea kutoa Hifadhi na kuwahudumia zaidi ya wakimbizi 250,000 katika Kambi mbalimbali.
Tumefarijika na kuanzishwa kwa Mradi huu muhimu kwani jamii hizo zimekuwa mstari wa mbele katika kugawa walichonacho kwa lengo la kuwasaidia wakimbizi hivyo tunawashukuru na tunadhani kuna u muhimu wa kuwasaidia katika utunzaji wa Mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya nchi pamoja na upatikanaji wa Nishati.
Amesema inapotokea Jamii inapokea Idadi kubwa ya wakimbizi kwa kipindi cha zaidi ya Muongo Mmoja, inakutana na changamoto kubwa zinazosababishwa na idadi kubwa ya watu ikiwemo uharibifu mkubwa wa Mazingira.
Uwepo wa wakimbizi mkoani Kigoma umeachangia kwa kiasi kikubwa katika kusababisha uharibifu mkubwa wa Mazingira kutokana na Ongezeko la Shughuli za kibinaadamu katika maeneo ya kambi pamoja na vijiji jirani na kambi hizo.
Naye Balozi wa Ufalme wa Ubelgiji nchini Tanzania Mhe. Peter Huyghebaert amesema Programu hiyo imeanzishwa mahususi ili kukabiliana na uharibifu mkubwa wa Mazingira uliofanyika katika Maeneo yanayohifadhi wakimbizi mkoani Kigoma.
‘’Kipaumbele chetu katika kutekeleza mradi huu ni kuzigusa Jamii zinazohifadhi wakimbizi kwa muda mrefu kwani maeneo yameathrika kimazingira kwa kiasi kikubwa hivyo tunalazimika kuanzisha mpango huu ili kukabiliana na Athari zinazosababishwa na Mabadiliko ya Tabia ya nchi’’ amefafanua Balozi Huygerbaert.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa