Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye amewataka wakazi mkoani hapa kuzingatia Sheria kwa kutovamia na kufanya shughuli za kibinaadamu katika maeneo tengefu ya Hifadhi za Mazingira ili kuifanya dunia kuwa sehemu salama kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo, alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mpeta Wilayani Uvinza Mkoani hapa, mara baada ya uzinduzi wa zoezi la usimikaji nguzo na mabango kwa ajili ya kubainisha mipaka ya Hifadhi ya chanzo cha Maji cha Mto Malagarasi, linalotarajiwa kuanza kutekelezwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika-Kigoma.
Amesema ongezeko la shughuli za kibinaadamu ikiwemo kilimo cha kuhama hama pamoja na ufugaji holela vimeendelea kusababisha athari kubwa za kimazingira, ambapo baadhi ya watu kwa makusudi wamekuwa wakiendesha shughuli hizo bila kujali mipaka inayowekwa na Serikali kwa lengo la kutunza mazingira.
‘‘Mbali ya kuwa ni chanzo kikuu kinachochangia Asilimia sabini ya Maji katika ziwa Tanganyika, Mto Malagarasi ni urithi wa Dunia kutokana na kuwa sehemu ya uhifadhi wa viumbe hai ambao wameanza kutoweka duniani kote, hivyo hatuna budi kuutunza’’ amesema Andengenye.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika Mkoa wa Kigoma Tamimu Mlimbo, amesema eneo linalotarajiwa kuwekewa mabango na usimikaji wa nguzo ili kuonyesha mipaka ya mto huo lina ukubwa wa Kilomita za mraba 42, likiwa limeathiriwa zaidi na shughuli za Kilimo na pamoja na ufugaji holela.
Amesema walishafanya vikao na wananchi wanaopakana na maeneo hayo kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa zoezi hilo pamoja na hatua zitakazochukuliwa na Serikali iwapo ukiukwaji wa Sheria za uhifadhi wa vyanzo vya maji utajitokeza katika maeneo yatakayobainishwa.
‘‘Kwa sasa wananchi watatengewa maeneo maalum ya kupita ili kunywesha mifugo yao kwa lengo la kutoathiri shughuli za ufugaji, aidha tumejipanga kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo ili kuyafanya maeneo ya hifadhi yabaki salama’’ amesema Mlimbo.
Mlimbo, amesisitiza kuwa maeneo owevu ni muhimu yahifadhiwe kwa sababu husaidia kuhifadhi maji yanapotokea mafuriko hivyo kupunguza uwezekano wa maji hayo kufikia makazi ya watu na kusababisha maafa pamoja na uharibifu wa mali.
Naye shija Magota ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, amesema walishajengewa uelewa juu ya umuhimu wa zoezi hilo hivyo watatoa ushirikiano kwa kutofanya shughuli zozote za kilimo na ufugaji katika maeneo yatakayobainishwa kuwa ni hifadhi ya Mto Malagarasi.
Wakazi hapa walikuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu maeneo yasiyotakiwa kulisha mifugo na kulima mazao mbalimbali, hivyo kwa sasa tumepata uelewa na tutajielekeza katika maeneo yaliyoruhusiwa kiserikali kufanya shughuli zetu za uzalishaji mali. Amesema Magota.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa