Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye amesema wananchi wanahitaji kupata taarifa za mara kwa mara na zenye uhakika kuhusu maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali mkoani Kigoma.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy pamoja na Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati wanaofadhili miradi ya kusambaza Nishati vijijini, walipomtembelea Ofisini kwake kwa Lengo la kujitambulisha pamoja na kuwasilisha Taarifa fupi ya hali ya Utekelezaji wa Miradi ya Umeme kwa Mkoa wa Kigoma.
‘‘Tunapotekeleza majukumu yetu ya kuwatumikia wananchi kuna kufikiwa au kutokufikiwa kwa Malengo, hivyo mnapotupatia taarifa za maendeleo ya kazi zenu inaturahisishia kuwapa wananchi taarifa sahihi na kuondoa tetesi au hali ya sintofahamu inayosababishwa na watu wasio na nia njema wanaoshindwa kuheshimu kazi nzuri zinazoendelea kutekelezwa na Serikali’’ amesema Mhe. Andengenye.
Aidha Mkuu wa Mkoa amepongeza kazi nzuri ya usambazaji wa huduma hiyo muhimu mkoani hapa, huku akiwaasa wananchi watumie fursa ya uwepo wa umeme katika maeneo yao kwa lengo la kuboresha hali ya uzalishaji mali na kujiinua kiuchumi.
Akitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa Umeme Mkoani Kigoma, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Hassan Saidy, amesema Miradi ya Umeme iliyopo kwenye Mpango wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023kimkoa ni pamoja na Ujazilizi fungu 2B ambapo jumla ya vitongoji 210 vilivyopo katika wilaya za Uvinza, Kasulu, Kakonko, Kigoma vijijini na Buhigwe vitanufaika.
Aidha ameitaja miradi mingine kuwa ni Mradi wa kupeleka Umeme kwenye vituo vya Afya 8 pamoja na pampu za Maji 17, mradi wa kupeleka Umeme sehemu za Migodi midogo, kilimo na aina zote za viwanda pamoja na maeneo yaliyo pembezoni mwa Mji na Majiji ambapo wilaya za Kigoma vijijini, Buhigwe, Kibondo, Kakonko, Uvinza na Kasulu zitanufaika.
‘‘Mpaka kufikia Novemba 2022, Jumla ya Vitongoji 883 kati ya 1,855 vya Mkoa wa Kigoma vimepelekewa Umeme huku vitongoji 972 ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo hatua za uhakiki wa taarifa na utekelezaji wake zinaendelea kufanyika ambapo pia utekelezaji utategemea upatikanaji wa Fedha’’ amesema Mhandisi Hassan.
Amesisitiza kuendendelea kushirikiana na wadau pamoja na uongozi wa mko katika kuhakikisha Miradi ya umeme vijijini inatekelezwa kwa mujibu wa mikataba inavyoelekeza ili kuharakisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa Maendeleo ya wananchi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa