Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi zake za kukabiliana na maadui Ujinga, Maradhi na Umasikini ili kuufanya Mkoa na Taifa kwa ujumla kuweza kuwa na Uchumi imara na kujitegemea.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Kigoma, ambapo amesisitiza jamii kujenga tabia ya kufanya kazi kwa bidi ili kujiimarisha kiuchumi.
Amesema iwapo Jamii itafanikiwa kukabiliana na maadui hao watatu na kila mtu kutekeleza wajibu wake kwa ufasaha, kujituma pamoja na kudumisha amani na utulivu, uchumi wa mwananchi mmoja mmoja utazidi kuimarika na kulifanya taifa kusonga mbele.
‘‘Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu anaendelea kuendesha mapambano dhidi ya maadui hao kwa kuboresha miundombinu mbalimbali inayoleta ufanisi katika utoaji wa huduma za jamii pamoja na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi’’ amesema Andengenye.
Andengenye amesema mkoa wa Kigoma unajivunia mapinduzi makubwa ya Miundombinu yanayoendelea kufanyika ikiwemo ukarabati wa Uwanja wa Ndege, Ujenzi wa Barabara mbalimbali kwa kiwango cha Lami, mkoa kuunganishwa na Umeme wa Gridi ya Taifa, uboreshwaji mkubwa wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, ujenzi wa vyuo vikuu pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Magharibi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Aidha katika kutekeleza shughuli mbalimbali zinazokwenda sambamba na maadhimisho hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amegawa miche zaidi ya 2000 ya zao la chikichi kwa wakazi wa Kata ya Machinjioni kisha kuhitimisha maadhimisho hayo kwa kushiriki kufanya usafi katika soko la Nazareti katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli amehimiza jamii wilayani humo kujenga Tabia ya kudumisha usafi ili kupunguza athari mbalimbali zinazoweza kusababishwa na maradhi na kupunguza nguvu kazi ya Taifa.
‘’Nashauri tabia hii ya kufanya usafi katika maeneo ya kutolea huduma za Umma na yale binafsi iwe endelevu, tusisubiri mpaka tupewe shinikizo au kutokea matukio bali tuifanye iwe tabia endelevu kwa usalama wa Afya zetu na wenzetu wanaotuzunguuka’’ amesema Kalli.
Maadhimisho hayo yametanguliwa na Mdahalo uliofanyika Desemba 8, 2023 uliolenga kuangazia mafanikio ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, uliofanyika katika Ukumbi wa Kigoma Social Hall Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa