Jumla ya Wapiga kura 1,333,911 wanatarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari la Wapigakura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Kigoma unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27, 2024 nchini.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Zoezi hilo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Mhe. Hassan Rugwa amesema jumla ya vituo 2252 vitatumika katika zoezi hilo kimkoa huku akisisitiza kuwa maandalizi ya zoezi hilo yamekamilika na kutoa wito kwa wakazi kujitokeza kujiandikisha ili kutopoteza haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka ili kuimarisha Demokrasia nchini.
Amesema Serikali ya awamu ya Sita imedhamiria kuimarisha misingi ya demokrasi ili wananchi waweze kupata viongozi bora watakaowajibika kwao katika kuhakikisha wanafikia malengo yao ikiwemo kusimamia mipango ya serikali kwa nia ya kuwaletea wananchi Maendeleo.
Upande wake Shehe Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Alhaji Hassan Kiburwa amesema kila mwananchi anapaswa kujiandikisha ili kupata kiongozi ambaye atapatikana kupitia maamuzi ya wananchi husika na kuepuka kuamuliwa kupata kiongozi wasiyemtaka.
Amewataka wakazi mkoani Kigoma kuhakikisha wanachagua viongozi wenye maadili mema na wachapakazi watakaomsaidia Mhe. Rais kusimamia shughuli za maendeleo na kutanguliza maslahi ya wanaowaongoza.
Padre George Mhanuka ambaye ni Paroko Msaidizi Parokia ya Kigoma amesema uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali nchini huchangia kuimarisha ustawi wa Jamii, Amani na Maendeleo kwa wakazi.
Amesema ni haki na wajibu wa kila mtanzania kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kutimiza matakwa ya kisheria ya nchi yanayowapa fursa wananchi kuchagua kiongozi kuendana na mahitaji yao.
Upande wake Bilantanye Bakeyemba Mkazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ameonesha kuridhishwa na maandalizi na utekelezaji wa zoezi hilo unaofanywa na serikali mkoani Kigoma.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt. Rashidi Chuachua, Viongozi wa dini pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya Siasa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa