WANANCHI MKOANI KIGOMA wenye sifa hususani makundi muhimu kama wanawake, watu wenye ulemavu na vijana tujitokeze kwa wingi kuchagua na kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa.
wa viongozi katika nchi ni utaratibu (mchakato) rasmi unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi kwa njia ya kuwapigia kura kuwachagua watu ambao wanawataka kuwaongoza kwa kipindi maalumu.
Uchaguzi ni utaratibu wa kawaida wa demokrasia wa kuwapata wawakilishi wa kisiasa ambao umekuwa ukitumika tangu karne ya 17.
Uchaguzi huwapa wananchi fursa ya kutoa mamlaka yao kwa kundi dogo la watu ili waweze kuunda serikali. Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inatamka kwamba, Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.
Tanzania, tuna aina tatu za msingi za uchaguzi zinazotumika kuwapata viongozi kulingana na mfumo wetu wa uchaguzi. Aina hizo ni uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Uchaguzi wa Wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano (Tanzania Bara) na Baraza la Wawakilishi (Tanzania Zanzibar), na Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa. Vyama vya Siasa kwa upande wao navyo huendesha chaguzi ambazo zinajulikana kwa jina la “uchaguzi wa msingi” zinazotumika kuwachagua wateuliwa wa vyama katika aina za uchaguzi ambazo zimetajwa hapo juu na pia kuwapata viongozi wa vyama husika kulingana na Katiba ya vyama vyao.
Kwa mujibu wa Ibara ya 6 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Serikali maana yake ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali za Mitaa na pia mtu anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya serikali yoyote.
Kwa mantiki hiyo basi katika utendaji wa shughuli za kiserikali Tanzania ina serikali za ngazi mbili; yaani serikali kuu (ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania) na serikali za mitaa. Kwa mujibu wa ibara ya 151(1), kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali za Mitaa maana yake ni vyombo vya kiserikali vilivyoundwa kwa mujibu wa ibara ya 145 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya kutekeleza madaraka ya umma.
Sheria ya Serikali za mitaa iliundwa mwaka 1982 chini ya Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sheria Na.7 ya Mwaka 1982 [Sura ya 287 ya Sheria za Nchi Marejeo ya Mwaka 2002] na Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sheria Na.7 ya Mwaka 1982 [Sura ya 288 ya Sheria za Nchi Marejeo ya Mwaka 2002]; Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Serikali za Mitaa zimeanzishwa kwa Sheria namba 3 ya mwaka 1986 iliyopitishwa na Baraza La Wawakilishi Zanzibar.
Serikali za Mitaa nchini zimeundwa kwa Mujibu wa Ibara ya 145 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Madhumuni na kazi za Serikali za Mitaa yameainishwa chini ya Ibara ya 146 ya Katiba.
Kwa mujibu wa Katiba ibara 146, Serikali za Mitaa ni vyombo vya haki na vyenye mamlaka ya kushiriki na kushirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma katika sehemu zao. Vyombo hivyo vinatakiwa viimarishe demokrasia na viwajibike kwa wananchi katika utoaji wa huduma na kuchochea maendeleo.
Uchaguzi wa viongozi wa Serikali ni hitaji la kikatiba na takwa la demokrasia. Kama inavyoeleweka demokrasia ni mfumo wa serikali ambapo wananchi wote ni sawa mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa juu ya masuala ya umma.
Wakati mwingine wananchi hushiriki moja kwa moja, hii ina maana kwamba wao hupiga kura moja kwa moja kwenye masuala kama vile sheria na katika uchaguzi. Wakati mwingine huwakilishwa na viongozi wao waliowachagua.
Nchi yenye demokrasia ya kweli huzingatia, kuhimiza na kuruhusu haki za kiraia na kisiasa kama vile uhuru wa kusema, uhuru wa kukusanyika, kutoa maoni, kuabudu na kushiriki kusisitiza utawala wa sheria, utawala wa walio wengi pamoja na kuheshimu haki za wachache.
Kwa mujibu wa Ibara ya 146(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali za Mitaa zitakuwa na majukumu ya kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika eneo lake, kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi, kuimarisha demokrasia katika eneo lake na kuitumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Siasa ya vyama vingi na demokrasia nchini zilianza mwaka 1992 baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa mwaka 1992. Baada ya kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa uchaguzi wote ukiwamo wa Serikali za Mitaa zilihusisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa