Muu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amelipongeza Shirika la World Vision kwa kutekeleza mradi wa kujenga miundombinu ya huduma za Afya kwa kujenga majengo ya Upasuaji na Wodi za Kinama, pamoja na na vifaa tiba katika Wilaya za Kakonko, Kibondo na Kasulu Mkoani Kigoma.
Andegenye amesema hayo wakati alipozindua rasmi majengo ya vyumba vya upasuaji na wodi ya wazazi katika kituo cha Afya Kagezi Wilayani Kibondo, uzinduzi huo umefanyika ukiwa unawakilisha uzinduzi wa vituo vingine vya Gwanumpu Wilaya ya Kakonko na Kimwanya Wilaya ya Kasulu.
Mradi wa Sustain Kigoma ni mradi uliotekelezwa kwa miaka minne Mkoani Kigoma ambao lengo lake lilikuwa kuboresha Afya ya uzazi, vijana na watoto kwa kuboresha mifumo ya upatikanaji na matumizi ya huduma bora za afya ya uzazi, vijana na watoto katika mkoa wa Kigoma. .
Mkuu wa Mkoa amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani kwa miaka mitano iliyokwisha ukiachilia mbali sekta nyingine Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika kuboresha Miundombinu ya Afya kwa kujenga zahanati, Vituo vya Afya, na Hospitali ili kurahisisha upatikana wa huduma bora kwa urahisi na gharama nafuu kwa Wananchi wa Mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa Ujumla.
Ninafurahi kuona kwamba World vision mmeonesha juhudi kubwa ya kuunga mkono nia ya Serikali katika kushiriki kwenye uimarishaji wa Miundombinu ya huduma za Afya kwa kutujengea Majengo ya Upasuaji na Wodi za Kinama. Hizi ni jitihada kubwa sana katika kusaidia Mkoa wa Kigoma kufikia lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vile vya watoto wadogo.
Amewaagiza Viongozi wa Serikali na Watendaji wakuu kwenye Mkoa na mamlaka za Serikali za Mitaa kuakikisha wanashirikiana ili kuona miradi hii inatunzwa na kulindwa kwa manufaa ya umma, “World Vision wameshamaliza kazi yao, sula la utunzaji kwa matumizi endelevu ni letu sisi watumiaji. Hivyo usimamizi wa karibu wa miradi hii kwenye maeneo yenu ni suala la Msingi sana” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Ameongeza kuwa fedha zilizotumika kutekeleza miradi hiyo ni fedha ya ziada kutoka kwa Wananchi wa Canada, hivyo ni vema kuona thamani ya upendo wao kwa kulinda na kutunza majengo, na vifaa vyote vilivyonunuliwa kwa ajili ya miradi hii.
Aidha nipende kutoa wito kwa Mashirikia mengine Mkoani Kigoma kuendelea kusaidi na kuunga mkono juhudi mbalimbali za Serikali siyo tu katika Afya bali hata katika maeneo mengine kama vile Elimu, Maji, Kilimo na maeneo mengine ambayo yanamgusa mwananchi moja kwa moja
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa