Serikali mkoani Kigoma imesaini mkataba kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za Awali za Mradi wa Hewa Ukaa katika Halmashauri za wilaya Kakonko, Kibondo na Kasulu.Mkataba huo unatarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya Ørsted Nature Based Solution A/S kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia wakimbizi la Denmark (DRC) kwa kipindi cha Miaka 30 kuanzia mwaka 2024, ambapo Jumla ya Hekta 500,000 zinatarajiwa kupandwa miti katika Halmashauri hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma mara baada ya kushudia utiliaji saini huo, Mkuu wa wilaya ya Kibondo Kanali Agrey Magwaza amesema taratibibu za kuyatambua maeneo lengwa katika wilaya hizo zilishafanyika na kazi inayoendelea ni kuwaelimisha wananchi kuhusu manufaa na hatua za utekelezaji mradi ili wawe na utayari wa kuupokea katika maeneo yao.
Amesema mradi huo ni shirikishi kwani kupitia mikutano baina ya wataalam wanaoratibu mradi na wananchi katika maeneo ambayo mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa, watakubaliana kutenga maeneo rasmi yanayomilikiwa na serikali za vijiji kwa jili ya utekelezaji.
Upande wake Mratibu wa Mradi Alfred Mageima amesema wamezilenga halmashauri hizo tatu katika Mkoa wa Kigoma kutokana na kupata athari kubwa za kimazingira zilizosababishwa na uwepo wa shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikifanywa na wakimbizi na kusababisha uharibifu mkubwa wa Mazingira.
Amesema kupitia mradi huo, Halmashauri hizo zitanufaika kwa kupata fursa za kuwezeshwa kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma mbalimbali za Jamii kama ujenzi wa shule, vituo vya kutolea Huduma za Afya, barabara pamoja kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Maji.
Mratibu huyo ameyataja malengo mahususi ya mikataba iliyosainiwa kuwa ni pamoja na kukubaliana na wakazi katika maeneo pendekezwa kwa ajili ya kuhuisha na kuhifadhi misitu itakayotambuliwa, ulinzi pamoja na ujumuishi katika mradi.‘’Katika halmashauri tulizozipendekeza, misitu imeharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi makubwa ya miti kama nishati kwa ajili ya kupikia, ufugaji uliopitiliza na kilimo cha kuhama hama hivyo kupitia mradi huu tutaanzisha hifadhi za ziada za misitu jambo litakalosaidia kuongeza miti kwa lengo la kudhibiti hewa ukaa katika maeneo yetu na duniani kwa ujumla’’ amesema Alfred.
Aidha amezitaja shughuli za Msingi zitakazotekelezwa kupitia mradi huo kuwa ni kuweka mpango endelevu wa matumizi bora ya Ardhi katika vijiji vitakavyohusika na mradi, kuwajengea uwezo wakazi na kuwawezesha katika kuanzisha, kusimamia na kutunza misitu na kuwawezesha katika kumudu stadi za utunzaji wa mazingira.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa