BALOZI WA INDIA NCHINI TANZANIA MHE. BINAYA PRADHAN AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA MKUU WA MKOA WA KIGOMA KAMISHNA JENERALI MSTAAFU WA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI MHE. THOBIAS ANDENGENYE, ALIPOMTEMBELEA OFISINI KWAKE MANISPAA YA KIGOMA/UJIJI.
Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema amedhamiria kuutangaza Mkoa wa Kigoma kiuwekezaji ili wafanyabiashara kutoka nchini mwake waweze kuzitambua Fursa na kufanya uwekezaji wenye Tija mkoani Kigoma.
Balozi Pradhan ametoa kauli hiyo aliposhiriki Mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara uliofanyika Mkoani hapa chini ya Chemba ya Wafanyabiashara, wenyeviwanda na Kilimo Tanzania(TCCIA).
Amesema amebaini uwepo wa fursa mbalimba za kiuwekezaji na zenye tija mkoani Kigoma na iwapo wawekezaji watatumia vizuri fursa hizo zitaweza kuwanufaisha wao binafsi pamoja, mkoa na nchi kwa ujumla.
Amefafanua kuwa, katika kuimarisha uhusiano mwema wa kibiashara na uwekezaji, Mpaka mwishoni mwa Mwaka 2022, nchi ya India ilifanikiwa kuwekeza zaidi ya Tril.10 katika shughuli mbalimbali za Biashara.
‘‘Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufungua milango na kutengeneza mazingira mazuri ya kiuwekezaj,i hali inayoendelea kusababisha ongezeko kubwa la wawekezaji kutoka nchini India kuja kuwekeza nchini Tanzania’’ amefafanua Balozi Pradhan.
Mbali ya uwekezaji kibiashara Balozi ameendelea kueleza kuwa, mahusiano ya nchi hizi mbili yaliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, yameendelea kuleta mazuri katika Sekta za Afya, Elimu, Madini, Maji na wananchi wa Nchi hizo kuishi kwa kuheshimiana hususani kwa raia wa nchi hiyo wanaoishi Tanzania.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amesema Mijadala na mazungumzo yanayofanyika baina ya wadau wa Maendeleo wa nchi hizi mbili katika kuangazia uwekezaji, italeta matokeo chanya kwa pande zote mbili.
Amefafanua kuwa, Mkoa wa Kigoma una fursa nyingi za kiuwekezaji zikiwemo zile za Kilimo cha Mazao ya Chakula na Biashara, Uwepo wa Eneo Maalum kwa ajili ya wawekezaji ''Kigoma Special Economic Zone''(KiSEZ), Biashara katika maeneo ya Mipaka zinazuhusisha nchi ya Tanzania na zile za Jirani, uwepo wa maeneo ya hifadhi za wanyama, uvuvi pamoja na Misitu.
Aidha Mkuu wa Mkoa amemsisitiza Balozi huyo na ujumbe wake kuwa wajumbe wema na kwenda kuusemea vizuri mkoa wa Kigoma katika uhalisia wake hususani kufuatia kuwepo kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya Usafiri na usafirishaji, Usalama, uimarishwaji mifumo ya wa Umeme, upatikanaji wa maji ya uhakika pamoja na mahusisano mema baina ya nchi ya Tanzania na zile za Jirani.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa